Jan 24, 2024 06:56 UTC
  • Vita vya Ukraine vyaubebesha Umoja wa Ulaya zigo zito la madeni

Umoja wa Ulaya umelazimika kubeba zigo zito la madeni kutokana na kuifuata kibubusa Marekani katika kuiunga mkono Ukraine kwenye vita na Russia.

Kitengo cha Huduma ya Utekelezaji wa Nje ya Ulaya (EEAS) kimegusia hatua ya nchi za bara hilo ya kuanza tena kuisheheneza Ukraine kwa silaha na kusema kuwa, Umoja wa Ulaya hivi sasa una zigo la deni la zaidi ya euro bilioni saba kutokana na kuipelekea silaha Ukraine.

Licha ya kwamba hali ya Ukraine iliyosambaratishwa vibaya na vita inazidi kuwa mbaya, lakini kitengo hicho cha EEAS cha Umoja wa Ulaya kinatayarisha mpango mpya wa kuipa Ukraine misaada zaidi ya kijeshi na kuruhusu wanachama wa umoja huo kukwepa kura ya turufu ya Hungary dhidi ya misaada yao ya kifedha kwa Kyiv.

Ukraine imejiingiza kwenye maangamizi kwa tamaa ya kusaidiwa na madola ya Magharibi

 

Kupitia mpango huo mpya, Umoja wa Ulaya unakusudia kuipa Ukraine msaada mwingine wa bilioni 50. Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma Hungary, ilitumia kura yake ya veto kuzuia kutolewa msaada huo wa kifedha kwa Kyiv. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary, Peter Ciarto, alisema siku ya Jumatatu kuwa nchi hiyo haitoshiriki katika kufadhili usambazaji wa silaha kwa Ukraine, lakini haiwezi kuingilia masuala ya nchi nyingine zinazonuia kushiriki.

Kwa upande wake, Joseph Burrell, mkuu wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya, amedokeza kuwa, tangu vita vya Ukraine vilipoanza, Umoja wa Ulaya umeshaipa Ukraine msaada wa kijeshi wa euro bilioni 30 na kuongeza kuwa, katika kipindi hicho, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zimetoa mafunzo kwa wanajeshi 40,000 wa Ukraine.

Tags