Hatua mpya za kivita na kichokozi za nchi zaMagharibi katika eneo la Asia Magharibi
Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ili kudumisha usalama, maslahi ya kiuchumi na kibiashara ya utawala huo katika Bahari Nyekundu, katikati ya mwezi wa Disemba mwaka jana, ilitangaza kuundwa muungano wa baharini lakini muungano huo haukuungwa mkono na nchi za Ulaya isipokuwa Uingereza.
Muungano huu ambao ilidai lengo lake ni kudumisha usalama katika Bahari Nyekundu (Bahari ya Sham) na mlango wa bahari wa Bab al-Mandab, umeshambulia maeneo mbalimbali ya Yemen, nchi ambayo tayari ilikuwa ikishambuliwa na muungano wa baadhi ya nchi za Kiarabu tokea mwaka 2015.
Katika hatua ya hivi karibuni ya kijeshi, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilitangaza kuwa Jumatatu iliyopita, Jeshi la Wanamaji la Marekani na Jeshi la Wanahewa la Uingereza, kwa msaada wa Australia, Bahrain, Canada na Uholanzi, lilishambulia maeneo 8 ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen. CENTCOM inadai kuwa maeneo yaliyolengwa ni yale yenye mifumo ya makombora, mifumo ya ulinzi wa anga, rada, vifaa na maghala ya silaha, ambayo baadhi yalikuwa chini ya ardhi.
Afisa mmoja wa jeshi la Yemen amesema: "Mashambulizi ya usiku wa Jumatatu yanaweza kutambuliwa kuwa mashambulizi makali zaidi dhidi ya Sana'a tangu kuanza kwa uchokozi wa madola ya Magharibi dhidi ya nchi yetu."
Imeripotiwa kuwa lengo la Marekani na washirika wake katika mashambulizi hayo ni kudhoofisha uwezo wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen wa kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya meli za kivita za Marekani na Uingereza, pamoja na meli za kibiashara zinazohusiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bahari Nyekundu, Mlango Bahari wa Bab al Mandab na Ghuba ya Aden.
Katika miezi michache iliyopita jeshi la Yemen lililenga meli kadhaa za utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu na mlango wa bahari wa Bab al-Mandab ili kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina ambao wanakabiliwa na vita vya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani katika Ukanda wa Gaza. Harakati ya Ansarullah imesisitiza kuwa itandeleza oparesheni zake Bahari Nyekundi hadi pale utawala wa Kizayuni utakapokomesha jinai zake dhidi ya taifa la Palestina.
Utawala wa Kizayuni ambao hauwezi kuzilinda meli zake ulikimbilia msaada wa Marekani kutatua tatizo hili. Lakini uundaji wa muungano mpya majeshi ya wanamaji unaoongozwa na Marekani haukufaulu pia. Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen anasema: "Lengo la muungano wa wanamaji ambao ulitangazwa na Washington ni kuilinda Israel na si meli za kimataifa. Amesisitiza kuwa nchi yake itajibu mashambulizi yoyote ya Marekani."
Mashambulio ya Yemen dhidi ya meli za kibiashara zinazoelekea katika bandari za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel, yamesababisha uharibifu mkubwa kwa Israel, ambayo zaidi ya asilimia 90 ya biashara zake za nje hutegemea bahari.
Wakati huo huo gharama za biashara ya baharini duniani (hasa kwa mataifa ya Magharibi) pia imeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Madai ya Marekani ni kwamba usalama wa usafiri wa baharini katika Bahari Nyekundu umekuwa hatarini kutokana na vitendo vya Wayemen. Hii ni katika hali ambayo ni wazi kwa watu wote kuwa, lengo halisi la muungano wa Marekani katika Bahari Nyekundu ni kulinda usalama wa Israel. Tangu kuanza kwa mashambulizi ya anga na ardhini ya Wazayuni dhidi ya ukanda wa Gaza, serikali ya Biden imekuwa ikiuunga mkono utawala wa Kizayuni kwa pande zote.
Washington inaamini kwamba, kuundwa muungano wa wanamaji katika Bahari Nyekundu, kutadhamini usalama wa Wazayuni.
Harakati za kijeshi za Marekani zinalenga kuzusha moto zaidi katika eneo la Asia Magharibi, na hilo linafanyika kwa mujibu wa matakwa haramu ya viongozi wa utawala wa Kizayuni.
Kuhusiana na suala hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian amesema katika taarifa yake mpya kwamba: "Tumetoa ujumbe na onyo zito kwa Wamarekani kwamba hatua yao ya pamoja na Waingereza katika Bahari Nyekundu na dhidi ya Yemen ni "kosa la kistratijia".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Wakati Marekani na Uingereza zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Yemen, picha za satelaiti zinaonyesha kuwa takriban meli 230 za biashara na mafuta zilikuwa zikisafiri katika Bahari Nyekundu; Hii ina maana kuwa wamepokea vyema ujumbe wa Wayemeni kwamba ni meli tu zinazokwenda kwenye bandari zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel ndizo zitakazozuiwa na Wayemen.
Suala jingine ni kwamba Marekani na Uingereza zimejaribu kuilaumu Iran kwa mashambulizi ya Wayemen katika Bahari Nyekundu. Kuhusiana na hilo, Brad Cooper, kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani alidai Jumatatu kwamba, Iran inahusika moja kwa moja na mashambulizi ya Ansarullah ya Yemen dhidi ya meli zinazohusiana na utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu.
Hata hivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani, amepinga madai yasiyo na msingi ya mashirika ya kijasusi ya Marekani kuhusu kuhusika kwa Iran katika mashambulizi ya Yemen dhidi ya meli za Israel katika Bahari Nyekundu.
Bagheri Kani amesema harakati ya Muqawama ina zana na uwezo wa kutosha na hutekeleza operesheni kulingana na maamuzi na uwezo wake.