Mahakama ya ICJ yatupilia mbali madai ya Ukraine dhidi ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i107876-mahakama_ya_icj_yatupilia_mbali_madai_ya_ukraine_dhidi_ya_russia
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imepinga takriban tuhuma zote zilizowasilishwa na Ukraine katika kesi ya kufadhili ugaidi dhidi ya Russia.
(last modified 2024-02-01T10:59:57+00:00 )
Feb 01, 2024 10:59 UTC
  • Mahakama ya ICJ yatupilia mbali madai ya Ukraine dhidi ya Russia

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imepinga takriban tuhuma zote zilizowasilishwa na Ukraine katika kesi ya kufadhili ugaidi dhidi ya Russia.

Akisoma uamuzi huo jana Jumatano kwa niaba ya majaji wenzake, Rais wa ICJ, Joan Donoghue amesema Russia imefungamana na vipengee vyote isipokuwa kimoja cha Hati ya Kimataifa ya Kupambana na Ufadhili wa Ugaidi.

Kyiv ilidai katika faili lake hilo kwamba Russia inafadhili makundi yanayotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine, na kwamba inaendeleza kampeni maalumu ya kuwafanyia ubaguzi Waukraine na watu wa jamii ya Tatar wanaoishi katika eneo la Crimea. 

Itakumbukwa kuwa, kisiwa cha Crimea kilijiunga na Russia mwaka 2014 baada ya kufanyika kura ya maoni ambapo zaidi ya asilimia 96 ya washiriki katika kura hiyo waliunga mkono suala hilo. Ukraine ingali inaitambua Crimea kama sehemu ya ardhi yake na kukitaja kisiwa hicho kuwa kilichovamiwa na kughusubiwa. 

Aidha mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imesema madai karibu yote ya Ukraine kwamba Russia imekiuka Hati ya Kimataifa ya Kukabiliana na Aina zote za Ubaguzi hayana msingi wala mashiko. 

Vita vya Ukraine

Uamuzi huo wa ICJ ni pigo maradufu kwa Ukraine wakati huu ambapo nchi hiyo ya Ulaya ina wasiwasi wa kupunguziwa misaada na waitifaki wake wa Magharibi. Rais wa Ukraine karibuni alikiri kuwa jeshi la nchi hiyo ni dhaifu mkabala wa Russia na kusema: Ulaya pekee haiwezi kuisaidia Ukraine dhidi ya Russia bila uungaji mkono wa Marekani.

Akihojiwa na televisheni ya Ujerumani, Rais Volodomir Zelensky wa Ukraine ameeleza bayana kuwa iwapo Marekani itapunguza misaada yake kwa Ukraine kuna uwezekano Ulaya ikashindwa kuisaidia Kyiv iwe ni kifedha na au kijeshi.