Feb 07, 2024 03:49 UTC
  • Nicaragua yazishtaki ICJ Ujerumani, UK, Uholanzi na Canada kwa kuisaidia Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina

Serikali ya Nicaragua imezishitaki Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Canada katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Kwa mujibu wa chaneli ya televisheni ya Al-Mayadeen, serikali ya Nicaragua imetangaza katika taarifa rasmi kwamba, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na Canada zinahusika katika ukiukaji mkubwa na wa kimpangilio wa Mkataba wa Kuzuia na Kutoa Adhabu kwa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari na Sheria za Kimataifa za Masuala ya Kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na serikali ya Nicaragua, nchi nne za Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Canada zimetakiwa pia ziache kupeleka silaha, risasi na teknolojia za kijeshi kwa utawala wa Kizayuni.
Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba, kwa vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza katika hukumu yake ya Januari 26, Israel inapaswa kuhakikisha inachukua hatua zinazohitajika ili kuzuia kuendelea mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Katika hatua nadra kushuhudiwa na katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 2024, serikali ya Afrika Kusini iliwasilisha mashtaka dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikiutuhumu utawala huo wa Kizayuni kwamba unafanya jinai ya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya Wapalestina 27,000, wengi wao wakiwa watoto, wanawake na wazee wameuawa shahidi tangu ulipoanza uvamizi na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.
Jinai za waziwazi za utawala wa Kizayuni dhidi ya binadamu zingali zinaendelea licha ya kufanyika maandamano makubwa kote duniani na kutolewa miito ya kusitishwa vita na serikali na wananchi wa mataifa mengi.../

Tags