NAM: Mashambulizi ya Israel huko Gaza yanapaswa kulaaniwa
Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kwa niaba ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kwamba: Kuendelea mashambulizi ya kikatili ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina hususan katika Ukanda wa Ghaza, kunapaswa kulaaniwa.
Zahra Ershadi aliyekuwa akizungumza kwa jana niaba ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, katika kikako cha Kamati Maalumu ya Hati ya Umoja wa Mataifa mjini New York amesoma taarifa ya jumuiya hiyo akisema: Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote inalaani vikali mashambulizi ya kikatili ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza na inasisitiza ombi la kusitishwa mapigano mara moja kwa sababu za kibinadamu katika eneo hilo na kulindwa wananchi wa Palestina.
Zahra Ershadi ameongeza kuwa, Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote inaeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na maonyo yaliyotolewa na maripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na inaitaka jamii ya kimataifa izuie mauaji hayo na kuchukua hatua zote muhimu za kukomesha ukatili huo.
Ni vyema kukumbusha hapa kuuwa jana Jumanne, Marekani ilitumia tena kura ya veto kupinga rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Algeria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, la kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Hii ni mara ya tatu kwa Marekani kutumia kura yake ya veto katika Baraza la Usalama kupinga azimio la kusitishwa vita vya maangamizi ya kizazi vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Karibu Wapalestina 30,000 wameuawa shahidi hadi sasa katika mashambulizi ya kikatili ya Israel huku wengine zaidi ya elfu 69 wakijeruhiwa.