Feb 28, 2024 03:46 UTC
  • Maandamano yafanyika Washington na Los Angeles US kumuenzi askari aliyejichoma moto kulalamikia jinai za Israel

Wamarekani wameandamana katika miji ya Washington na Los Angeles kumuenzi mwanajeshi wa nchi hiiyo aliyejichoma moto kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulalamikia jinai za kinyama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi hao madhulumu.

Aaron Bushnell askari wa Jeshi la Anga la Marekani aliyekuwa na umri wa miaka 25, alionekana kwenye mkanda wa video aliojirekodi akichukua hatua ya kujichoma moto mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington kupinga na kulalamikia uungaji mkono wa Ikulu ya White House kwa mauaji ya wazi ya kimbari yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghazza.
Bushnell alifariki dunia licha ya kukimbizwa hospitalini kutokana na kuungua vibaya sana.

 

Katika mkanda huo wa video uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii, askari huyo wa jeshi la Marekani alisikika akisema: "sitashiriki tena katika mauaji ya kimbari" huku akipaza sauti na kusema "Palestina Huru."

Televisheni ya Al-Mayadeen imeweka kwenye mtandao wa X picha za maandamano yaliyofanyika mbele ya ubalozi mdogo wa utawala wa Kizayuni mjini Los Angeles kulalamikia kifo cha mwanajeshi wa Marekani anayeunga mkono Palestina na kupinga mauaji ya kimbari.

Chaneli ya Fox 5 pia imerusha hewani taswira za mkusanyiko wa waungaji mkono wa Palestina mbele ya mahali alipojichoma moto askari huyo wa jeshi la anga la Marekani mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington.

Mashinikizo yameongezeka dhidi ya serikali ya Marekani kuitaka iunge mkono usitishaji kamili wa mapigano katika Ukanda wa Ghazza licha ya msimamo wa rais wa nchi hiyo Joe Biden wa kupinga suala hilo.

Wakati Marekani inajaribu kuonyesha mbele ya macho kuwa inajali masuala ya kibinadamu ili kupunguza mashinikizo ya maoni ya umma kutokana na ushiriki wake wa moja kwa moja katika vita vya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina, Jumanne ya wiki iliyopita, ilichukua kwa mara ya tatu hatua ya kupigia kura ya veto azimio la usitishaji vita wa haraka katika Ukanda wa Ghazza, ili kuendelea kuunga mkono jinai za utawala huo ghasibu.

Jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina zimeamisha dhamiri na hisia za walimwengu, ambapo katika maeneo yote ya dunia watu, serikali na taasisi mbalimbali za kimataifa zimetoa wito wa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.../

Tags