Apr 16, 2024 02:13 UTC
  • Bunge la Marekani laionya Washington isijiingize kwenye vita vya kijeshi na Iran

Mkuu wa Kamati ya Kijasusi ya Bunge la Marekani amewaonya viongozi wa Washington kuhusu matokeo mabaya ya kujiingiza katika hatua yoyote ya kijeshi inayoweza kuchukuliwa dhidi ya Iran.

Gazeti la Washington Times limemnukuu Michael Ray Turner, Mkuu wa Kamati ya Kijasusi ya Bunge la Marekani ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican kutoka jimbo Ohio akitoa onyo hilo na kusisitiza kuwa, hivi sasa serikali ya Marekani inapaswa kujiepusha kikamilifu na hatua yoyote ya kijeshi inayoweza kuchukuliwa dhidi ya Iran.

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Bunge la Marekani vile vile amesema, Washington inapaswa kuiainishia Iran mistari yake myekundu ambayo itaweza kulinda usalama wa Israel. Amesema, Marekani haipaswi kujiingiza kwenye hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran kwani matokeo yake ni ya hatari na hayatabiriki.

Vilevile amedai kuwa, pamoja na yote hayo, lakini kwa kuzingatia hali tete iliyopo kwenye eneo la Asia Magharibi hivi sasa, waitifaki wa Marekani kama utawala wa Kizayuni na Ukraine wataendelea kuhitaji msaada wa Washington.

Usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 14 Aprili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran (SEPAH) waliushambulia moja kwa moja utawala wa Kizayuni kutokea kwenye ardhi ya Iran kwa makombora na droni yaani ndege zisizo na rubani ikiwa ni kujibu jinai ya Israel ya kushambulia ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus.