Mvua kali za mafuriko zaua watu wasiopungua 168 Pakistan na Afghanistan
Apr 20, 2024 10:41 UTC
Watu wasiopungua 168 wamepoteza maisha katika matukio yaliyosababishwa na mvua, baada ya mvua kali na mafuriko kuikumba Pakistan na nchi jirani ya Afghanistan.
Watu wapatao 100 wamefariki dunia na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika matukio yaliyosababishwa na mvua, baada ya mvua kali na mafuriko kuyakumba maeneo ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Pakistan.
Kulingana na Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Majanga (NDMA), mvua kubwa imesababisha mafuriko katika mikoa ya Khyber Pakhtunkhwa, Balochistan na Punjab na Jammu na Kashmir zinazosimamiwa na Pakistan, zinazojulikana pia kama Azad Jammu na Kashmir.
Kulingana na ripoti ya karibuni ya NDMA, hadi kufikia sasa, watu 98 wameripotiwa kupoteza maisha na wengine 89 wamejeruhiwa katika maeneo hayo, katika kipindi cha juma lililopita kutokana na miundo kuporomoka.
Nyumba zipatazo 3,261 zimeharibiwa na nyingine 536 zimebomoka kikamilifu.
Mafuriko makubwa na utelezi wa ardhi pia vimeharibu barabara na madaraja katika maeneo ya milimani ya Khyber Pakhtunkhwa na Balochistan.
Wakati huo huo, Wizara ya Kudhibiti Majanga ya Afghanistan imesema, watu wasiopungua 70 wamefariki na wengine 56 wamejeruhiwa kutokana na mvua kubwa na mafuriko yaliyotokea katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo katika wiki iliyopita.
Likinukuu ripoti ya wizara hiyo, Shirika la Habari la Bakhtar limetangaza kuwa, mafuriko hayo yameharibu pia sehemu za nyumba 2,627 au kubomoa kikamilifu, mbali na kuangamiza mifugo zaidi ya 600.
Shirika la Hali ya Hewa la Afghanistan limetabiri kuwa msimu wa sasa wa mvua utaendelea hadi Jumapili.../
Tags