Waziri wa Ulinzi wa Russia: Ukraine imeshapoteza karibu askari nusu milioni
Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergey Shoigu amesema, hasara za kijeshi ilizopata Ukraine za kuuawa askari wake tangu Februari 2022 hadi sasa zimefikia karibu wanajeshi 500,000.
Akihutubia mkutano wa mawaziri, Shoigu amefafanua kuwa, vikosi vya Russia vina mkakati vinaotekeleza kwenye mstari wa mbele wa mapigano na vinawarudisha nyuma wapinzani wao; na akaongeza kuwa, shinikizo hilo la vikosi hivyo linawazuia wanajeshi wa Kiev na kuwafanya wabaki kwenye hali ya kujihami.
Waziri wa Ulinzi wa Russia amezungumzia pia msaada wa kijeshi wa zaidi ya dola bilioni 60 unaotarajiwa kutolewa na Marekani kwa Kiev na akabainisha kuwa, hatua hiyo inalenga "kuzuia kusamabaratika" kwa vikosi vya Ukraine, lakini akatabiri kwamba, fedha hizo hazitaathiri kwa kiasi kikubwa hali katika medani ya vita, kwa kuwa nyingi zake zitaenda kwenye sekta ya uundaji silaha ya Marekani.
Shoigu ameongezea kwa kusema: "mamlaka za Marekani zinasema kwa kejeli kwamba Waukraine watakufa katika vita vya kupigana na Russia kwa ajili ya maslahi yao".
Hii ni katika hali ambayo, maafisa wa Washington na Kiev wametamka kuwa kuilipa Ukraine ipigane na Russia ni afadhali kuliko Marekani kupigana ana kwa ana na Russia.
Msaada wa mabilioni ya dola za Marekani uliombwa na Ikulu ya White House tangu miezi kadhaa iliyopita lakini ulipitishwa hatimaye na Baraza la Wawakilishi siku ya Jumamosi baada ya kuafikiwa na Spika wa baraza hilo Mike Johnson.../