May 06, 2024 05:16 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Mei 6

Huu ni mukhtasari wa baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbalimbali za dunia…..

Iran yatwaa ubingwa wa voliboli Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya ubingwa wa voliboli ya ufukweni ya Asia kwa vijana wenye chini ya miaka 19. Mabarobaro wa Iran walitawazwa mabingwa baada ya kuiduwaza Lebanon kwa alama 2-0 za 21-12, 21-12 katika mchuano wa fainali uliopigwa katika ukumbi wa michezo wa shule ya jamii ya Ban Nong Ya Ma mjini Roi Et, nchini Thailand. Iran iliizaba Australia katika mchezo wa nusu fainali na kujitatia tiketi ya kushiriki fainali ya mashindano hayo yaliyoivutia nchi 32 za bara Asia.

 

Huku hayo yakijiri, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na timu ya voliboli ya wanafunzi wa Iran ambayo hivi karibuni iliibuka kidedea katika mashindano ya dunia nchini Serbia. Katika mkutano huo wa Jumatano hapa jijini Tehran, Ayatullah Ali Khamenei amewapongeza wanafunzi hao wa Kiirani kwa kuitoa kimasomaso Jamhuri ya Kiislamu kwenye mashindano hayo ya kimataifa.

Kabla ya hapo, Rais Ebrahim Raisi wa Iran aliipongeza timu hiyo ya voliboli ya wanafunzi wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ushindi wa alama 3-0 dhidi ya Ujerumani. Katika ujumbe wake a tahania siku ya Jumatatu, Sayyid Raisi alisema: Taifa la Iran linaona fakhari kwa ushiriki wenu aali na matokea ya kuridhisha kwenye mashindano hayo ya voliboli. Iran iliizaba Ujerumani 3-0 katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama ISF World School Volleyball Championship yaliyofanyika Belgrade, Serbia baina ya Aprili 20-28, 2024.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Voliboli la Iran limesaini hati ya maelewano katika yake na utawala wa Kisultani wa Oman. Rais mpya wa shirikisho hilo, Milad Taghavi alienda Muscat, mji mkuu wa Oman kutia saini mkataba huo maelewano wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa mchezo huo baina ya nchi mbili hizi.

 

Na timu ya mchezo wa sataranji ya vijana wenye chini ya miaka 18 ya Iran imeibuka ya pili kwenye mashindano ya majiji ya Asia ya mwaka huu 2024. Vijana hao wa Kiirani wameibuka washindi wa pili kwa kuzoa jumla ya alama 16 kwenye mashindano hayo ya kieneo. Majiji ya Ulaya pia yalishirii kwenye mashindano hayo yaliyofanyika katika jiji la Khanty Mansiysk, Russia. Timu ya mabanati wa Kiirani imemaliza ya sita kwenye mashindao hayo yaliyofunga pazia lake Jumatatu iliyopita, kwa kuchota alama 9.

Azam nusu fainali Kombe la Shirikisho CRDB

Klabu ya Azam FC ya Tanzania imefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au ukipenda 'CRDB Bank Federation Cup'. Hii ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 ilipochuana na Namungo FC katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam. Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo wa Robo Fainali yalifungwa na viungo, Mkodivaa Kipré Tiagori Emmanuel Junior Zunon dakika ya 10, Iddi Suleiman ‘Nado’ dakika ya 15, Feisal Salum Abdallah dakika ya 19 na Mgambia, Gibril Sillah katika dakika ya 52.

 

Bao la kufitia machozi la Namungo FC lilifungwa na kiungo Ayoub Semtawa dakika chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza. Azam FC sasa itamenyana na Coastal Unión katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la TFF. Union hiyo karibuni iliitoa Geita Gold kwa kuichapa bao 1-0 katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga. Nusu Fainali nyingine ni baina ya mabingwa watetezi, Yanga dhidi ya Ihefu ambayo iliitoa Mashujaa FC kupitia upigaji matatu kwa mabao 4-3 baada ya sare ya 0-0 mjini Singida. Yanga imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania mara tatu sawa na Simba huku Azam FC ikichukua taji hilo mara moja.

Ligi ya EPL; Ni Arsenal au City?

Klabu ya Arsenal inahitaji pointi mbili pekee katika mechi zake mbili ilizosalia nazo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ili itawazwe kuwa ya pili, ikiwa ubingwa utaiponyoka. Gunners wikendi iliichabanga Bournemouth mabao 3-0 wakiupipigia nyumbani Emirates. Mabao ya Wabeba Bunduki kwenye mchezo huo yalifungwa na Bukayo Saka (penati), Leandro Trossard na Decla Rice. Arsenal kwa sasa ikiwa na pointi 83 inaweza kusanya pointi 89 iwapo itashida mechi zote mbili zilizosalia msimu huu, dhidi ya Man U na Everton.

Huku hayo yakiarifiwa, Liverpool siku ya Jumapili iliishukia vibaya Tottenham Hotspur na kuaiadhibu mabao 4-2. Mabao ya Liverpool wakiupigia nyumbani Anfield yalifungwa na Mohammed Salah, Andrew Robertson, Cody Gakpo na Harvey Elliot. Liverpool ambayo imefikisha alama 78 ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa igi, sasa inasubiri kutoana udhia na Aston Villa mnamo Mei 13 na kisha Wolves mnamo Mei 19.

Katika upande mwingine, Man City ambayo wikendi iliilaza Wolves mabao 5-1 inatazamia kuwinda ubingwa kupitia vipute dhidi ya Fulham mnamo Mei 11, Tottenham mnamo Mei 14 na hatimaye West Ham United hapo Mei 19. Aidha Jumapili, Chelsea ambayo katika wiki za karibuni imekuwa ikiboronga, iliinyoa kwa chupa West Ham kwa kuinyeshea mabao 5-0.

……………….MWISHO…………

 

Tags