ICJ itasikiliza kesi kuhusu uvamizi wa Israel dhidi ya Rafah
https://parstoday.ir/sw/news/world-i111768-icj_itasikiliza_kesi_kuhusu_uvamizi_wa_israel_dhidi_ya_rafah
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) itafanya vikao kujadili hatua mpya za dharura kuhusu uvamizi wa Israel katika mji wa kusini wa Rafah katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
(last modified 2024-05-15T00:55:29+00:00 )
May 15, 2024 00:55 UTC
  • ICJ itasikiliza kesi kuhusu uvamizi wa Israel dhidi ya Rafah

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) itafanya vikao kujadili hatua mpya za dharura kuhusu uvamizi wa Israel katika mji wa kusini wa Rafah katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Mahakama hiyo imesema vikao vya siku ya Alhamisi na Ijumaa vitashughulikia ombi kwa ICJ kuagiza hatua zaidi za dharura dhidi ya Israel kuhusu mashambulizi yake dhidi ya Rafah.

Hatua hizo ni sehemu ya kesi inayoendelea ambayo Afrika Kusini iliiwasilisha katika Mahakama ya ICJ mnamo Desemba 2023 ikiishutumu Israel kwa kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wakati wa vita vya vya kikatili Gaza.

Mahakama ya ICJ mapema mwaka huu iliuamuru utawala wa Israel kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake ili kuzuia mauaji ya halaiki huko Gaza. Amri hiyo ya ICJ ni sehemu ya uamuzi wake wa muda kuhusu hatua za dharura katika kesi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel.

Nchi kadhaa zikiwemo Misri, Uturuki na Colombia sasa zimeomba rasmi kujiunga na kesi dhidi ya Israel katika ICJ.

Rais wa Colombia pia ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati ya kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel kutokana na mauaji ya kimbari huko Gaza.

Gustavo Petro amesema Benjamin Netanyahu hatakomesha mauaji ya halaiki na hii ina maana ya kuwepo haja ya kutolewa hati ya kukamatwa kwake.

Rais wa Colombia pia amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzisha kikosi cha kulinda amani katika Ukanda wa Gaza.