Waislamu Uingereza washtushwa na kuteuliwa Bi. May kama Waziri Mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i11212-waislamu_uingereza_washtushwa_na_kuteuliwa_bi._may_kama_waziri_mkuu
Waislamu nchini Uingereza wameshtushwa na kuteuliwa Bi. Theresa May kama Waziri Mkuu kutokana na sera zake haribifu kwa jamii ya Waislamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2016 02:00 UTC
  • Waislamu Uingereza  washtushwa na kuteuliwa Bi. May kama Waziri Mkuu

Waislamu nchini Uingereza wameshtushwa na kuteuliwa Bi. Theresa May kama Waziri Mkuu kutokana na sera zake haribifu kwa jamii ya Waislamu nchini humo.

Taarifa zinasema May anatazamiwa kuendeleza sera zake dhidi ya Waislamu akiwa katika nafasi ya kiongozi wa Uingereza.

May ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alichukua hatamu za uongozi Uingereza siku ya Jumatano kutoka kwa David Cameron na ameahidi kupambana na kile alichokitaja kuwa ni misimamo mikali kwa kustawisha thamani na mila za Uingereza hasa uhuru wa maoni.

Hii ni haki ambayo aliwapokonya wanachuo Waislamu uhuru wa maoni katika vyuo vikuu vya Uingereza mwezi Novemba mwaka 2014 wakati alipopendekeza Sheria ya Kukabiliana na Ugaidi. Sheria hiyo ambayo ilipitishwa katika bunge la Uingereza iliwazuia wanafunzi Waislamu kubainisha mitazamo yao katika mihadhara na semina kwa hofu ya kutajwa kuwa wenye misimamo mikali. Wakati May akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Waislamu Uingereza waliandamwa na kupelelezwa na maafisa maalumu wa polisi waliotumwa katika mitaa yao. Ni kwa sababu hii ndio mwaka jana Tume ya Haki za Binadamu za Kiislamu ikamtaja May kuwa 'Mtu Mwenye Chuki Dhidi ya Uislamu wa Mwaka' au Islamophobe of the Year.

Waislamu Uingereza wanakubaliana kwa kauli moja kuwa, vitendo vya May akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani vilipelekea chuki na hujuma dhidi ya Waislamu kuwa kitu cha kawaida katika jamii na matokeo yake ni kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa Waislamu milioni tatu nchini Uingereza.