Slovenia: Kulitambua taifa la Palestina ni wajibu wa kimaadili
Waziri wa Mambo ya Nje wa Slovenia amesema kuitambua Palestina kama nchi huru ni jukumu la kimaadili.
Tanja Fajon amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Jazeera na kusema kuwa, mchakato wa nchi yake kulitambua rasmi taifa huru la Palestina upo katika marhala ya mwisho.
Amesema hatua ya Slovenia kujiunga na muungano wa nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zipo mbioni kuitambua Palestina ni mkakati muhimu wa kidiplomasia. "Kulitambua taifa la Palestina ni wajibu wa kimaadili," ameongeza Fajon.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Slovenia amebainisha kuwa, kitendo cha nchi yake kuitambua Palestina kinaibua masuali nyeti kuhusu ushawishi wa mataifa madogo katika diplomasia ya dunia, na uwezo wa nchi hizo kubadilisha mikondo ya kijiopolitiki iliyokita mizizi.
Slovenia inaelekea kuitambua nchi huru ya Palestina katika hali ambayo, siku chache zilizopita, Ireland, Norway na Uhispania zilitangaza pia kulitambua rasmi taifa la Palestina, jambo ambalo limeukasirisha sana utawala haramu wa Israel.
Hivi karibuni, Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya sambamba na kusema kuwa nchi nne wanachama wa EU ambazo ni Uhispania, Ireland, Slovenia, na Malta zipo mbioni kulitambua taifa huru la Palestina, alidokeza kuwa, yumkini Ubelgiji na nchi nchi nyingine kadhaa za Ulaya zikafuata mkumbo huo wa kulitambua taifa la Palestina.
Harakati hizo za kulitambua taifa huru la Palestina zinaendelea katika hali ambayo, azimio lililopendekezwa na nchi za Kiarabu kuhusu uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa liliidhinishwa kwa wingi wa kura mnamo tarehe 10 Mei katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.