Slovenia imelitambua rasmi taifa la Palestina
Bunge la Taifa la Slovenia limepiga kura kuunga mkono kuitambua Palestina kama nchi huru. Hayo yameelezwa na Spika Urska Klakocar Zupancic mbele ya bunge hilo.
Kulingana na maelezo yaliyotolewa na Zupancic wabunge 53 walishiriki katika upigaji kura huo.
Spika wa Bunge la Slovenia ameongeza kuwa, wabunge 52 walipiga kura ya kuunga mkono hoja ya kuitambua nchi huru ya Palestina na hakuna mbunge aliyepiga kura ya kupinga uamuzi huo na kwa msingi huo nchi hiyo imetambua rasmi Palestina kama nchi huru.
Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, Serikali ya Slovenia ilipitisha uamuzi wa kuitambua Palestina kama nchi huru tarehe 30 Mei na kulipeleka suala hilo bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa na bunge.
Mnamo Mei 22, nchi za Uhispania, Ireland, na Norway zilitangaza uamuzi wao wa kuitambua Palestina kama nchi huru.
Hadi sasa zaidi ya nchi 140 kati ya 193 za Umoja wa Mataifa (UN) zinaitambua Palestina kama nchi huru.