UN yaiweka Israel kwenye Orodha ya Aibu ya wanaoua watoto
https://parstoday.ir/sw/news/world-i112676-un_yaiweka_israel_kwenye_orodha_ya_aibu_ya_wanaoua_watoto
Umoja wa Mataifa umeongeza jeshi la Israel kwenye "orodha ya aibu" ya kila mwaka ya wahalifu wanaoua watoto.
(last modified 2024-06-08T00:38:30+00:00 )
Jun 08, 2024 00:38 UTC
  • UN yaiweka Israel kwenye  Orodha ya Aibu ya wanaoua watoto

Umoja wa Mataifa umeongeza jeshi la Israel kwenye "orodha ya aibu" ya kila mwaka ya wahalifu wanaoua watoto.

Gilad Erdan, balozi wa utawala wa Israel katika Umoja wa Mataifa, alifahamishwa rasmi kuhusu uamuzi huo ambao umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, siku ya Ijumaa.

Orodha hiyo imeambatanishwa na ripoti kuhusu watoto na mizozo ya kivita ambayo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa huwasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kila mwaka.

Ripoti hiyo inahusu ukatili kama vile kuua na kulemaza watoto, kuwafanyia unyanyasaji wa kijinsia, kuwateka nyara au kuwasajili watoto kwenye vita, kuzia misaada ya watoto, na kulenga shule na hospitali.

Orodha hiyo imetangazwa wakati utawala haramu wa Israel unaendeleza vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana.

Watoto wa Gaza baada ya hujuma ya utawala haramu wa Israel

Mashambulizi hayo ya kijeshi ya Israel hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 36,731 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Siku ya Ijumaa, serikali ya Palestina katika Ukanda  Gaza iliripoti kuwa, tangu kuanza mashambulizi hayo, jeshi la Israel limeua zaidi ya watoto 15,517.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa zaidi ya watoto 17,000 wa Gaza hadi sasa pia wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili.

Takriban watoto 3,500 wa Gaza wamekuwa wakipambana na utapiamlo ambao umesababishwa na vita hivyo.