Jun 16, 2024 12:41 UTC
  • Maelfu waandamana Scotland kulaani jinai za Israel Gaza

Maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu wa Scotland, Glasgow kushiriki maandamano ya kulaani jinai za Israel na kutangaza kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, waandamanaji hao wenye uraia tofauti wameshiriki kwa wingi maandamano hayo licha ya vizingiti na mbinyo wa vyombo vya usalama vya serikali ya UK.

Waandamanaji hao wameonyesha kuchukizwa kwao mno na jinai za Israel dhidi ya wanawake na watoto watoto wadogo wasio na hatia wa Palestina na kushutumu uzembe wa Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama katika kushughulikia maafa ya Gaza. 

Mataifa kadhaa ya Ulaya na Asia yameendelea kushuhudia maandamano makubwa kwa siku kadhaa mtawalia ya kutaka kusitishwa mara moja uvamizi na jinai za Israel huko Gaza na na kuruhusu kuingia misaada ya kibinadamu. Mji mkuu wa Denmark, Copenhagen, hivi karibuni ulishuhudia pia maandamano makubwa, ambapo waandamanaji walizunguka katika mitaa mingi, wakiimba nara za kutaka kusitishwa mara moja kwa jinai hizo na kutoa mwito wa kushtakiwa viongozi wa utawala huo ghasibu wakiwataja kuwa wahalifu wa kivita.

Maandamano kama hayo yalishuhudiwa hivi karibuni pia katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin ambapo waandamanaji wameitaka serikali yao kusitisha ushirikiano na Israel huku wakiitaka pia jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.