Putin aitembelea Korea Kaskazini baada ya miaka 24
Rais Vladimir Putin wa Russia amewasili nchini Korea Kaskazini katika ziara ya nadra inayoonyesha kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais Putin amepokewa na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un katika uwanja wa ndege wa Pyongyang, na wawili hao walikumbatiana kabla ya kuelekea katika nyumba ya wageni ya Kumsusan ambako Putin atakaa.
Putin ambaye anafanya ziara yake ya kwanza Korea Kaskazini katika kipindi cha miaka 24, ameeleza katika taarifa iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari vya serikali saa chache kabla ya kuwasili kwake, kuwa anashukuru uungaji mkono wa Korea Kaskazini kwa oparesheni maalumu ya kijeshi ya Russia ndani ya ardhi ya Ukraine.
Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini limeelezea mkutano kati ya Putin na Kim Jong Un kama tukio la kihistoria linaloonyesha uimara wa urafiki wa dhati na umoja kati ya mataifa hayo mawili.
Vyombo vya habari vya Korea kaskazini vinaripoti kuwa viongozi hao wawili wamejadili namna ya kuimarisha mahusiano na kile wanachokitaja kubadilishana mawazo.
Pia inatarajiwa kuwa wawili hao watatia saini makubaliano mbalimbali, kuanzia uchumi hadi mikataba ya kiusalama.
Agenda kuu ya mazungumzo ingawa – weledi wa mambo wanasema - litakuwa ni kujadili jinsi mataifa yaliyotengwa zaidi yanavyoweza kuimarisha uhusiano wao wa kijeshi, wakati Putin anatazamia kuongeza usambazaji wake wa silaha na silaha kwa vita vyake nchini Ukraine.