Jul 11, 2024 02:33 UTC
  • Benjamin Netanyahu
    Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa utawala wa Israel, Benjamin Netanyahu amefuta mpango wa kushukia katika moja ya nchi za Ulaya kabla ya kuendelea na safari yake ya kwenda Marekani, akihofia kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inajiandaa kutoa waranti wa kumtia nguvuni kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Televisheni ya Kizayuni ya Kan imeripoti kuwa, Ofisi ya Netanyahu imefuta mpango wa hapo awali wa Waziri Mkuu huyo wa utawala katili wa Israel kusimama kwa muda ama katika Jamhuri ya Czech au Hungary, licha ya nchi hizo kutambuliwa kuwa waitifaki wa utawala wa Kizayuni.

Mbabe huyo anayeongoza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza  atasafiri moja kwa moja hadi Washington, huku ndege yake akibeba abiria wachache tu wa 'dharura'.

Nchi nyingi duniani, zikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Afrika Kusini, Colombia na hata Palestina yenyewe, zimekuwa zikiishinikiza mahakama ya ICC yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imkamate Netanyahu kwa kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Netanyahu anatazamiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti la Marekani mnamo Julai 24, sambamba na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Joe Biden wa Marekani katika Ikulu ya White House.

Mahakama ya ICC

Viongozi mbali mbali wa Marekani akiwemo Seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders wamewakosoa vikali viongozi wa Kongresi ya nchi hiyo, kwa kumualika Netanyahu 'mtenda jinai' kuhutubia kikao cha pamoja cha Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti la Marekani.

Sanders anasema, "Netanyahu ni mtenda jinai ya kivita, hastahiki kualikwa kuhutubia kikao cha pamoja cha Kongresi ya Marekani. Bila shaka sitahudhuria (kikao hicho)."

 

Tags