Aug 12, 2024 10:45 UTC
  • UN: Maandamano ya kupinga utalii Uhispania yanaweza yakasambaa katika eneo

Afisa Mkuu wa Mradi wa Utalii Endelevu katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO ametahadharisha kuwa maandamano ya kupinga utalii wa halaiki ambayo yameikumba Uhispania hivi majuzi yanaweza yakaenea katika eneo zima.

Katika miezi ya hivi karibuni, maelfu ya Wahispania wameandamana dhidi ya utalii wa halaiki katika miji ya Malaga, Mallorca, Gran Canaria, Granada na Barcelona. Watu kutoka sehemu zote maarufu nchini Uhispania, ambayo imeorodheshwa kama nchi ya pili kwa kutembelewa zaidi ulimwenguni, wanazungumza dhidi ya uvamizi wa watalii ambao wanasema umeifanya miji yao isiweze kuishika.

Akinukuliwa na gazeti la The Guardian la Uingereza Afisa Mkuu wa Mradi wa Utalii Endelevu Peter DeBrine amesema: "tunachokiona ni kuvukwa kizingiti cha uvumilivu katika maeneo haya; kwa hakika ni hali ya kujaribu kurejesha mlingano wa hali hiyo. Mlingano kwa sasa umeparaganyika kikamilifu."

Mnamo mwezi uliopita wa Julai, shirika la habari la Reuters liliwanukuu polisi wa eneo hilo wakieleza kwamba maandamano ya kupinga utalii yaliyofanyika huko Palma de Mallorca, Uhispania yalihudhuriwa na karibu watu 10,000, ambapo mmoja wa waandamanaji aliliambia shirika hilo la habari kwamba watu wanataka watalii wachache, akitaja kupanda kwa bei kubwa na matatizo ya huduma za umma yanayowakabili wenyeji katika kisiwa hicho.

Katika maandamano mengine yaliyofanyika Julai pia waandamanaji wanaopinga utalii huko Barcelona waliwanyunyizia wageni bunduki za maji na kushikilia mabango yaliyosomeka "Watalii rudini makwenu" na "Hamkaribishwi."

DeBrine amesema, vitendo hivyo vinavyoshuhudiwa "vimevuka mpaka na havina ulazima," lakini akasisitiza kuwa "havitaondoka mpaka kuwepo na uchukuaji wa hatua fulani." Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kubadilishwa mtazamo, ambapo watoaji maamuzi wataanza kuchukua hatua za kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo, huku akionya kuwa kuna uwezekano wa kutiliwa maanani wa maandamano hayo kuenea nje ya Uhispania.../

Tags