Aug 15, 2024 07:55 UTC
  • Wanachuo wanaoitetea Palestina 'wakaribisha' kujiuzulu Rais wa Chuo Kikuu cha Columbia

Rais wa Chuo Kikuu cha Columbia Minouche Shafik alitangaza kujiuzulu jana Jumatano, takriban miezi minne baada ya chuo hicho kushuhudia maandamano ya wananchuo waliokuwa wakilalamikia vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel huko Gaza.

Shafik amesema ametoa tangazo hilo ili uongozi mpya uweze kuteuliwa kabla ya muhula mpya kuanza mnamo Septemba 3, wakati ambapo wanafunzi wa chuo hicho wameapa kuanza tena maandamano.

Usimamizi wa Chuo Kikuu cha Columbia umetangaza kuwa, Katrina Armstrong, mkuu wa kitivo cha matibabu cha chuo hicho atahudumu kama rais wa mpito, kurithi mikoba ya Shafik.

Vuguvugu la 'Apartheid Divest' la Chuo Kikuu cha Columbia, ambalo ni kundi linaloratibu maandamano hayo, limekaribisha hatua ya kujiuzulu Shafik, lakini limesema hatua hiyo haipaswi kuzuia juhudi zao za kutaka chuo hicho kijitenge na makampuni yanayounga mkono jeshi la Israel na kukalia kwa mabavu maeneo ya Wapalestina.

"Tunatumai kuwa (Chuo Kikuu cha) Columbia hatimaye kitateua rais ambaye atasikiliza wanachuo badala ya kufurahisha Bunge la Congress na wafadhili," amesema Mahmoud Khalil, mmoja wa viongozi wakuu wa kundi hilo.

Rais wa Chuo Kikuu cha Columbia Minouche Shafik aliyejiuzulu

Ikumbukwe kuwa, Aprili mwaka huu, wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani walianzisha maandamano ya kupinga jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina; maandamano yaliyochochea cheche za mwamko katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo na hata katika nchi za Ulaya, licha ya mbinyo wa polisi.

Tags