Uingereza inataka kuboresha uhusiano wake na Umoja wa Ulaya
Keir Starmer Waziri Mkuu wa Uingereza amefanya safari katika miji ya Berlin na Paris kwa lengo la kuboresha uhusiano na Umoja wa Ulaya.
Ufaransa na Ujerumani ambazo ni nchi mbili kubwa katika Umoja wa Ulaya ndio nguvu ya uendeshaji ya umoja huo. Hitilafu kuhusu namna Uingereza inavyopasa kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika nyanja mbalimbali zimeacha mwanya katika uhusiano wa EU na Uingereza. Hatimaye mwezi Disemba mwaka 2020 Uingereza ilijitoa katika Umoja wa Ulaya baada ya duru ya mivutano mikubwa baada ya nchi hiyo mwaka 2016 kuendesha kura ya maoni kuhusu kujitoa au kuendelea kusalia ndani ya EU (Brexit).
Keir Starmer alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwezi Julai mwaka jana baada ya kukishinda chama cha Conservative. Waziri Mkuu wa Uingereza kutoka chama cha Labour alisema baada ya kushinda uchaguzi kuwa miaka minne baada ya nchi yake kujitoa katika Umoja wa Ulaya, sasa anajipanga kuhuisha upya uhusiano ambao umeathiriwa na mivutano na mizozo ya miaka kadhaa kuhusu masharti ya Brexit.

Tofauti na mtangulizi wake Rishi Sunak, ambaye alisafiri kwenda Ujerumani miezi 18 baada ya kuwa Waziri Mkuu, Starmer kwa upande wake amesafiri mjini Berlin na kisha Paris mara tu baada ya kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza. Baada ya kukutana na Olaf Scholz Kansela wa Ujerumani mjini Beriln na Rais Emanuel Macron huko Paris, Waziri Mkuu huyo wa Uingereza amezungumzia suala la kusaini mikataba ya ushirikiano na Ujerumani na Ufaransa katika nyanja mbalimbali, hasa katika nyanja za ulinzi na usalama. Starmer amesema baada ya kuzungumza na Macron katika Ikulu ya Elizer kwamba: "Katika mazungumzo yetu tumejaribu kurekebisha uhusiano na kuhakikisha tunatekeleza dhamira yetu nambari moja ambayo ni kukuza uchumi kati ya kazi tutakazokuwa nazo'. Akiwa ziarani Ujerumani, Starmer amesema: "Hatukusudii kufuta Brexit bali tunatazamia kuidhinisha makubaliano mapya na Ujerumani kwa lengo la kuimarisha uhusiano na nchi hii katika nyanja mbalimbali."
Baada ya mazungumzo na Scholz, Waziri Mkuu wa Uingereza ameesema anataraji kuwa watafikia mapatano na Ujerumani hadi kufkikia mwishoni mwa mwaka huu. Layla Moran Msemaji wa sera za nje wa chama cha Liberal Democrat cha Uingereza ameeleza kuwa mazungumzo kati ya waziri mkuu huyo na Kansela wa Ujeruman ni hatua chanya baada ya miaka kadhaa ya kuharibiwa na wahafidhina uhusiano kati ya Uingereza na Ulaya. Ameongeza kuwa, hata hivyo serikali mpya ya Uingereza inapasa kuwa jadi na kudhihirisha azma yake thabiti ili kuboresha uhusiano imara na waitifaki wao wa Ulaya. Msemaji wa sera za nje wa chama cha Liberal Democrat cha Uingereza ameendelea kubainisha kuwa hatua hiyo inapasa ianze kutekelezwa kwa kukubaliana na Mpango wa Kuwahamisha Vijana, ambao utawapa vijana fursa ya kuishi na kufanya kazi kwa urahisi katika bara zima la Ulaya.
Kuanza tena mazungumzo kuhusu mapatano baada ya Brexit kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, kujiunga tena na soko moja la Umoja wa Ulaya au Umoja wa Forodha na pia kuwepo uwezekano wa kuwarejeshea raia haki yao ya kuingia katika mipaka yote ya Ulaya na Uingereza ni kati ya masuala ambayo serikali ya Starmer inapasa kuyajadili ili kuimarisha uhusiano wa nchi yake na EU. Uhusiano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya, hata wakati nchi hiyo ilipokuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, wakati wote uliathiriwa na uhusiano wake na Marekani. Keir Starmer kiongozi wa chama cha Labour na Waziri Mkuu wa Uingereza anataka kuwepo uhusiano wa mlingano kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya na Marekani kinyume na Wahafidhina. Khususan hivi sasa ambapo kuna uwezekano wa kuingia tena madarakani Trump huko White House iwapo atashinda uchaguzi ujao wa mwezi Novemba.
