Mahakama ya Kilele Brazil yaamuru kupigwa marufuku nchi nzima mtandao wa kijamii wa X
Jaji wa Mahakama ya Kilele ya Brazil ameamuru kupigwa marufuku na kusimamishwa kazi za mtandao wa kijamii wa X katika kona zote za nchi hiyo ya Amerika ya Latini.
Uamuzi huo unafuatia shutuma kwamba mtandao wa X unaomilikiwa na bilionea wa Marekani, Elon Musk, unapuuza na kudharau mara kwa mara amri na sheria za mahakama ya Brazil.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya amri hiyo, Jaji Moraes wa Mahakam ya Kilele ya Brazil amesema: "Kutotii amri za mahakama mara kwa mara, kwa kufahamu na kwa makusudi na kudharau faini za kila siku zinazotolewa na mahakama, pamoja na kuweka mazingira ya kukwepa adhabu kwa chaka la 'ardhi isiyo na sheria' yaani mitandao ya kijamii, ni miongoni mwa sababu za kupigwa marufuku mtandao wa kijamii wa X nchini Brazili.
Mahakama ya Kilele ya Brazil pia imesisitiza kuwa, mtandao wa X umekuwa ukitoa na kueneza matamshi ya chuki na ya ubaguzi wa rangi na kuingilia taratibu za demokrasia nchini Brazil.
Tarehe 28 mwezi ulioisha wa Agosti, Jaji Moraes alimpa Musk saa 24 kuteua wakili wake nchini Brazil, akionya kwamba kutofanya hivyo kungesababisha kupigwa marufuku kikamilifu mtandao huo X nchini humo lakini Musk alidharau amri hiyo ya mahakama.
Serikali ya Brazil imepiga marufuku akaunti kadhaa za mtandao wa X, zikiwemo za washirika na wafuasi wa Rais wa zamani Jair Bolsonaro ambaye anatuhumiwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya Rais Luiz Inacio Lula da Silva.