Sep 15, 2024 12:10 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN atoa indhari kuhusu hatari ya Akili Mnemba (AI)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa indhari kuhusu Akili Mnemba au Bandia (Artifcial Intelligence) na kusisitiza kuwa endapo itaachwa bila kudhibitiwa, hatari inazosababisha zinaweza kuwa na athari kubwa kwa demokrasia, amani na utulivu.

Guterres ametoa tahadhari hiyo katika salamu zake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inayoadhimishwa Septemba 15 kila mwaka.
Katika salamu hizo, Katibu Mkuu wa UN amesema: “siku hii ni fursa ya kusisitiza umuhimu wa kuzingatia uhuru wa kujieleza, uhuru wa raia na utawala wa sheria, kuhakikisha uwepo wa taasisi zinazowajibika na kulinda na kukuza haki za binadamu.”
Ameendelea kueleza kwamba, fursa hiyo ni muhimu sana katika mwaka ambao zaidi ya nchi 50 zinazowakilisha nusu ya idadi ya watu duniani zinafanya uchaguzi.
Guterres amesema, hata hivyo, haki na maadili hayo yanashambuliwa kote ulimwenguni na kubainisha kuwa “uhuru unaminywa, nafasi ya raia inapungua, mivutano inazidi na kutoaminiana kunaongezeka.”
Maudhui ya Siku ya Demokrasia ya mwaka huu inaangazia akili mnemba au bandia AI, kama chombo cha utawala bora.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

Kwa muktadha huo, Guterres ameeleza katika ujumbe wake kwamba, ikiachwa bila kudhibitiwa, hatari zinazoletwa na akili mnemba zinaweza kuwa na athari kubwa kwa demokrasia, amani na utulivu. Ameongeza kuwa hiyo inaweza kuanza kwa kusambaa habari potofu na za uongo, kuenea kwa kauli za chuki na matumizi ya kile kinachojulikana kama batili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amehitimisha ujumbe wake kwa kusema: “katika Siku hii ya Kimataifa ya Demokrasia, tuendelee kufanya kazi ili kujenga ulimwengu jumuishi zaidi, wenye haki na usawa”…/

Tags