Ongezeko kubwa la ubaguzi dhidi ya Waislamu barani Ulaya
(last modified Fri, 25 Oct 2024 07:41:24 GMT )
Oct 25, 2024 07:41 UTC
  • Ongezeko kubwa la ubaguzi dhidi ya Waislamu barani Ulaya

Uchunguzi mpya umebaini kuwepo 'ongezeko kubwa na lenye kutia wasiwasi" la ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu barani Ulaya hasa baada ya utawala haramu wa Israel wa kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wanaodhulumiwa katika Ukanda wa Gaza.

Utafiti huo uliochapishwa Alhamisi na Shirika la Umoja wa Ulaya la Haki za Msingi (FRA) uligundua kuwa karibu nusu ya Waislamu barani Ulaya walikabiliwa na ubaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ripoti ya FRA imeongeza kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa kasi, hasa katika mwaka uliopita huku taharuki zikiongezeka Asia Magharibi,  ambapo sasa  "ni vigumu zaidi kuwa Muislamu katika Umoja wa Ulaya."

Utafiti huo, ambao ulifanywa kabla ya utawala wa Israel kuanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza zaidi ya mwaka mmoja uliopita mapema Oktoba 2023, ulihusisha zaidi ya nchi kumi za Umoja wa Ulaya ambapo zaidi ya Waislamu 9,600 walihojiwa kati ya Oktoba 2021 na Oktoba 2022.

Ripoti ya FRA imeongeza kuwa watu barani Ulaya, wanawake na watoto , walilengwa sio tu kwa ajili ya imani yao ya kidini, bali pia rangi ya macho, nywele na ngozi zao, pamoja na sifa zingine za mwili.

Waislamu milioni ishirini na sita wanaishi katika Umoja wa Ulaya unaojumuisha zaidi ya asilimia 5 ya wakazi milioni 448 wa nchi za umoja huo.