Hofu ya ghasia za baada ya uchaguzi Marekani, usalama waimarishwa
Usalama umeimarishwa kote marekani hasa mjini Washington D.C. huku kukiwa na hofu ya kuibuka ghasia baada ya matokeo ya uchaguzi wa rais unaofanyika leo Novemba 5.
Kikosi cha Siri cha kumlinda rais kimeweka uzio mpya wa chuma wa mita 2.5 kuzunguka jengo la White House na Idara ya Hazina, pamoja na makazi ya Makamu wa Rais Kamala Harris.
Vizuizi vya muda vilivyoadikwa, "Mstari wa Polisi: Usivuke" pia viliwekwa karibu na Ikulu ya Marekani.
Kikosi hicho aidha kimechukua hatua kali za usalama nje ya ukumbi wa mikutano wa West Palm Beach, Florida, ambapo mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump anatazamiwa kuweko katika usiku wa uchaguzi.
Hatua hizo zinakuja huku kukiwa na wasiwasi wa kuibika ghasia kama zile zilizoibuka siku chache baada ya uchaguzi wa rais mwaka 2020 na pia kabla ya kuapishwa rais wa Marekani mnamo Januari 2021. Wakati huo wanamgmabo wenye kitikadi kali wa Trump walipinga matokeo ya uchaguzi wa urais na kuibua ghasia.
Rais huyo wa zamani wa Marekani alidai kwamba alishinda uchaguzi wa urais wa 2020 na kwamba kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa wapiga kura.
Wafuasi wa Trump walivamia Jengo la Capitol tarehe 6 Januari 2021 wakati kikao cha wabunge wa congress kilipokuwa kimekaa kuidhinisha ushindi wa Biden
Shambulio la Capitol lilisababisha vifo vya watu kadhaa. Trump alishtakiwa kwa juhudi zake za kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020 huko Washington na Georgia.