Kushindwa tena Wazayuni, mara hii katika mitaa ya Amsterdam
(last modified Mon, 11 Nov 2024 04:35:21 GMT )
Nov 11, 2024 04:35 UTC
  • Kushindwa tena Wazayuni, mara hii katika mitaa ya Amsterdam

Kufuatia dharau na matusi ya mashabiki wa Kizayuni dhidi ya bendera ya Palestina baada ya kumalizika mechi ya kandanda kati ya Ajax Amsterdam na Maccabi ya Tel Aviv, vijana wanaounga mkono Palestina wamepambana vikali na Wazayuni.

Kama ilivyo kawaida ya matukio mengi kama hayo huko Ulaya, kwanza simulizi ya Wazayuni ndiyo ilipewa kipaumbele katika vyombo vya habari vya Ulaya. Katika simulizi za duru zenye mafungamano na Wazayuni, waungaji mkono  wa Palestina ndio kwanza waliwashambulia mashabiki wa timu ya soka ya utawala wa Israel. Pampoja na hayo ushahidi wa kuaminika unaonyesha kinyume cha simulizi hizo za Wazayuni, viongozi wa serikali na wanasiasa wanaoiunga mkono Israel nchini Uholanzi. Mechi ya Alhamisi usiku kati ya "Ajax ya Amsterdam" na "Maccabi ya Tel Aviv" ilifanyika katika fremu ya vilabu vya Ligi ya Ulaya. Inasemekana kuwa Wazayuni wapatao 3,000 walikwenda uwanjani kushabikia timu ya Maccabi, ambapo 57 kati yao walikamatwa kabla ya kumalizika kwa mchezo huo kutokana na vurugu zao. Mashabiki wa Kizayuni katika mitaa ya Amsterdam kabla ya kuanza kwa mchezo huo walipiga nara za kichopchezi kama vile "Hakuna tena shule huko Gaza, kwa sababu hakuna hata mtoto mmoja aliyesalia huko" na " Acheni jeshi lishinde ili liwaangamize Waarabu" na pia kuchanachana na kuichoma moto bendera ya Palestina.

Gazeti  la The Guardian limekiri kwamba ripoti zilizopo zinaonyesha kwamba mashabiki wa timu ya Israel kwanza waliwachokoza wakazi wa eneo hilo na kuchoma bendera ya Palestina na kisha kupiga nara za chuki dhidi ya Waarabu. Pia, vyombo vya habari vimechapisha picha ya pasipoti ya mmoja wa mashabiki anayedaiwa kuwa "raia" wa klabu ya Maccabi Tel Aviv, ambayo inaonyesha kuwa yeye ni mmoja wa askari wa jeshi la Israel. Ripoti ya EuroNews inasema katika ripoti yake kwamba: 'Wafuasi kadhaa wa timu ya kandanda ya Israel walichanachana bendera ya Palestina ambayo ilikuwa imetundikwa kwenye madirisha ya nyumba za mji wa Amsterdam.' Kitendo hicho kiliwakasirisha baadhi ya waungaji mkono wa Palestina na kuibua mapigano kati yao. Video za mashabiki wa Kizayuni zinawaonyesha kwa pamoja wakipiga nara za kichochezi na chuki dhidi ya Waarabu na Wapalestina.

Waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni huko Amsterdam wakichanachana bendera ya Palestina

Klabu ya Maccabi ya Tel Aviv ina mashabiki wa Kizayuni waliofurutu ada zaidi katika utawala wa Kizayuni, jambo linalowafanya wafahamike kwa tabia hiyo ya kihuni na uabuaji ghasia na fujo katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na dunia nzima kwa ujumla.

Wakati huo huo, radiamali kuhusiana na matukio ya Amsterdam imefichua kwa mara nyingine tena kilele cha udanganyifu, hadaa, undumakuwili na ubaguzi wa rangi unaofanywa na serikali za Magharibi zinazodai kutetea haki kibinadamu.

Benjamin Netanyahu, mchinjaji wa watu Gaza, amempigia simu waziri mkuu wa Uholanzi kufuatia matukio ya Amsterdam, ambayo amedai kuwa ni chuki dhidi ya Mayahudi, na kumtaka achukue hatua kali kwa ajili ya kukabiliana na suala hilo haraka iwezekanavyo. Utawala wa Kizayuni umetangaza kutuma ndege mbili kwa ajili ya kuwarudisha nyumbani mashabiki hao wachochezi wa timu ya Maccabi. Dick Schoof, Waziri Mkuu wa Uholanzi pia amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba amefuatilia kwa hofu kubwa vurugu hizo. Amesema: "Mashambulizi haya ya chuki dhidi ya Mayahudi wa Israel hayakubaliki kabisa. Ninawasiliana na pande zote kuhusu suala hilo." Ursula von der Leyen, Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya, pia amesema kwamba baada ya kuzungumza na Waziri Mkuu wa Uholanzi, ameeleza kusikitishwa kwake na mashambulizi hayo aliyodai kuwa ni ya chuki yaliyolenga raia wa Israel mjini Amsterdam.

Hii ni pamoja na kuwa tangu mwaka mmoja uliopita Wazayuni wamewaua kikatili watu 44,000 wasio na hatia huko Gaza, na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, thuluthi mbili ya wahanga hao ni wanawake na watoto. Lakini viongozi wa serikali za Magharibi wanaodai kutetea haki za binadamu wanahalalisha uhalifu huo wote dhidi ya binadamu kwa kisingizio cha kujilinda Israel, ambapo Marekani na serikali za Ulaya zinaisaidia kwa hali na mali serikali ya Netanyahu na kushirikiana nayo kwa karibu katika mauaji ya halaiki dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina na sasa huko Lebanon. Wakati huo huo zinadai kuwa kuwatetea watu hao wanaodhulumiwa katika nchi zao ni kinyume na ubinadamu.

Kama ambavyo vita vya Gaza na mapambano ya kupigiwa mfano ya muqawama wa Palestina yamedhihirisha wazi sura ya ukatili wa utawala wa Kizayuni katika fikra za wananchi wa nchi za Magharibi, hivi sasa unafiki wa serikali za Magharibi pia umefichuka wazi kwa watu wa nchi hizo. Hivi sasa, hakuna mtu yeyote barani Ulaya anayeogopa kuwatetea watu wa Palestina, na kadiri nchi za Magharibi zitakavyojaribu kuongeza uungaji mkono wao kwa utawala huo bandia wa Israel na kudai kuwa ukosoaji dhidi ya magaidi wa Kizayunini ni chuki dhidi ya Mayahudi, ndivyo zitakavyokabiliwa na jibu kali zaidi kutoka kwa raia wao zenyewe.