Hasira isiyo na mfano wake dhidi ya Wazayuni barani Ulaya
Jinai za kutisha zinazofanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza na Lebanon katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita zimekuwa na natija muhimu duniani hususan katika fikra za raia wa nchi za Magharibi, ambapo zimefichua sura halisi ya jinai na ubaguzi unaofanywa na utawala bandia wa Israel.
Bila shaka Wazayuni na waungaji mkono wao katika nchi za Magharibi bado wanaiita hasira hiyo dhidi ya Wazayuni kuwa ni chuki dhidi ya Israel na Mayahudi. Mkuu wa Jumuiya ya Mayahudi wa Ulaya alisema katika mkutano mmoja huko Poland kwamba: "Tunashuhudia kiwango cha wendawazimu cha chuki dhidi ya Israel huko Ulaya."
Tovuti ya habari ya Ynet imeandika kuhusu kikao hicho kwamba: "Washiriki wa mkutano huo wote wameingiwa na hofu kubwa ambapo kuhani Menachem Margolin, Mkuu wa Jumuiya ya Mashirika ya Kiyahudi ya Ulaya, amesema: Hali ya Wayahudi barani Ulaya kwa sasa ni mbaya sana, kila baada ya dakika 15 tunashuhudia kitendo cha chuki dhidi ya Wayahudi barani Ulaya, duru zote za Wazayuni ziko katika hali ya tahadhari, na hili limetufanya tuwaombe viongozi wa Umoja wa Ulaya watangaze hali ya hatari kwa muda wa miezi sita kwa ajili ya kukabiliana na jambo hili."
Wazayuni wa Marekani na Ulaya hutumia vibaya madai ya chuki dhidi ya Uyahudi kama chombo cha kukandamiza ukosoaji wowote dhidi ya uvamizi, uchokozi na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa muda wa miaka 76 sasa.
Kabla ya Oktoba mwaka jana, hatua yoyote ya kuwakosoa Wazayuni nchini Marekani iliambatana na adhabu kali kama vile kufungwa jela, kupigwa faini, kufukuzwa kazini na kutengwa wanafikira huru wenye misimamo ya kuukosoa utawala wa Israel na Wazayuni. Kwa kisingizio na madai bandia ya Mayahudi kuuliwa na Wajerumani katika Vita vya Pili vya Dunia Wazayuni wanataka kulipiza kisasi cha mauaji hayo ambayo hayakufanywa na Wapalestina kwa kuwaua kikatili Waislamu huko Palestina. Kwa msingi huo, kila sauti ya kupinga na kukosoa Wazayuni inadaiwa katika nchi za Magharibi kuwa ni chuki dhidi ya Uyahudi.
Kwa msingi wa siasa hizo za Wazayuni, serikali za Ulaya zimekuwa zikiita kila jinai inayofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina kuwa ni katika hatua ya kujilinda tawala huo. Kabla ya mwaka mmoja uliopita, zilikuwa zikikandamiza kila sauti ya upinzani na ukosoaji dhidi ya utawala huo pandikizi na uungaji mkono kwa watu wa Palestina. Lakini baada ya Oktoba mwaka jana ambapo Wazayuni walianza kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza, hali ya mambo imebadilika kabisa Ulaya ambapo sasa matukio makubwa yanashuhudiwa barani humo na Marekani.
Kuhani Margolin amedai kwamba wimbi la chuki dhidi ya Wayahudi ambalo linaenea Ulaya leo linaweza kuyaathiri makundi mengine katika nchi nyingine za dunia. Amesisitiza kuwa leo hii tunaona hali hii ya chuki ikienea mitaani na mashuleni miongoni mwa wanafunzi na kila sehemu barani Ulaya. Jinai za kutisha zinazofanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza zimezipelekea taasisi za kimataifa na watetezi wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi kuguswa na mauaji ya kimbari yanayofanywa kila siku dhidi ya Wapalestina.
Aidha chombo cha Wazayuni cha kukandamiza na kutumia madai ya 'chuki dhidi ya Mayahudi' kama mbinu ya kuficha jinai zao mbele ya watu wa Wamagharibi, hakina tena taathira kama ilivyokuwa katika miaka ya huko nyuma. Hata baadhi ya viongozi wa mataifa ya Ulaya wamelazimika kidhahiri kutoa matamshi ya kutaka vita vya Gaza visimamishwe mara moja ikiwa ni katika kudhihirisha sura zao za kinafiki na za kindumakuwili kuhusiana na suala zima la haki za binadamu.
Hii leo si Waislamu wanaoishi barani Ulaya pekee, bali watu mbalimbali barani humo wanawaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kutangaza hadharani kuchukizwa kwao na Wazayuni wetendajinai. Mfano wa wazi kuhusu kadhia hiyo ni msimamo uliochukuliwa hivi karibuni na baadhi ya wafuasi wa vuguvugu la ufeministi barani Ulaya. Katika mkutano wa Watetezi wa Wanawake nchini Ujerumani, Annalena Charlotte, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani na mwanachama wa Chama cha Kijani, alikosolewa vikali kutokana nahatua yake ya kutowaunga mkono wanawake wa Palestina.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya wanawake nusu milioni katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na uhaba wa chakula, ambapo 175,000 pia wanakabiliwa na hatari kubwa kwa afya zao. Katika miongo 2 iliyopita, hakuna vita vingine ambavyo vimekuwa na idadi kubwa ya wanawake na watoto waliouawa katika kipindi cha mwaka mmoja kama ilivyoshuhudiwa katika vita vya Gaza. Jarida la Marekani la "Jacobin" linaashiria mkutano wa wanaharakati wa masuala ya wanawake nchini Ujerumani, na kusema hata kama sera za ufeministi zimeandikwa katika siasa za mambo ya nje za Ujerumani, lakini sera hizo hazijawahi kwenda kinyume na haki za wanawake kama inavyofanyika hivi sasa nchini humo.
Kwa hiyo muqawama na uungaji mkono kwa wananchi madhulumu wa Palestina na kuchukizwa walimwengu na jinai za Wazayuni ni suala lililoenea ulimwenguni kote. Hata washirika wa karibu wa utawala bandia wa Israel hawaamini tena maelezo yanayotolewwa na Wazayuni katika kuhalalisha mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina. Ukosoaji wa Wazayuni umeenea sana kiasi kwamba serikali za Ulaya haziwezi tena kukandamiza sauti za malalamiko na ukosoaji dhidi ya Wazayuni kwa kisingizio cha eti chuki dhidi ya Uyahudi.