Taifa kubwa lenye mamia ya maelfu ya watu wasio na makazi
Hali ya kiuchumi na kijamii imekuwa ngumu zaidi kwa raia wa Marekani, na idadi ya watu wasio na makazi katika nchi hiyo imefikia rekodi ya kihistoria katika miaka ya hivi karibuni.
Idadi ya watu wasio na makazi nchini Marekani inazidi kuongezeka huku serikali ya nchi hiyo ikiendelea kutoa misaada ya silaha na zana za kijeshi kwa utawala haramu wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya Marekani imetangaza katika taarifa yake kwamba: Kufuatia mzozo wa ukosefu wa nyumba za bei nafuu, kupanda kwa mfumuko wa bei na kutokuweko ongezeko la kutosha la mishahara, idadi ya watu wasio na makazi nchini humo imefikia 771,480. Idadi hiyo ina maana kwamba, kila watu 10,000 nchini Marekani 23 kati yao hawana makazi.
Taarifa ya Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya Marekani imeeleza kuwa, idadi ya watu wasio na makazi nchini Marekani imefikia rekodi ya kihistoria.
Kadhalika taarifa hiyo imeongeza kuwa, wakati idadi ya wasio na makazi nchini humo ilifikia zaidi ya watu 650,000 mnamo Januari 2023 na idadi hii imefikia watu 771,480 mnamo Januari mwaka huu 2024 na hilo ni ongezeko la zaidi ya 18%.

Kwa mujibu wa wizara hiyo pamoja na mambo kama vile mgogoro wa nyumba za gharama nafuu, kupanda kwa mfumuko wa bei na ongezeko lisilo la kutosha la mishahara nchini Marekani, mgogoro wa afya na majanga ya kimaumbile sambamba na ukosefu wa ajira pia yameathiri ongezeko la idadi ya watu wasio na makazi katika nchi hiyo na hivyo kupelekea kushadidi malalamiko ya raia.
Kuhusiana na hili, Mtandao wa uchambuzi wa Commecial Risk umetangaza kuwa, Marekani ilipata ongezeko la 30% la migomo na maandamano ya vyama vya wafanyakazi na vibarua katika sekta mbalimbali katika mwaka uliopita.
Ripoti ya Taasisi ya Tathmini ya Bima ya Makampuni ya Chaucer pia inaonyesha kuwa, sababu ya maandamano na migomo mingi nchini Marekani katika mwaka mmoja uliopita ni kuongezeka kwa mzozo wa kiuchumi katika nchi hiyo.
Hali hii imeigubika Marekani katika hali ambayo, taifa hilo limetumia mamia ya mabilioni ya dola katika vita na operesheni za kijeshi katika maeneo tofauti ya ulimwengu kama vile Afghanistan na Iraq kutokana na sera zake mbaya ulimwenguni. Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa fedha kwa Ukraine katika vita na Russia na muungaji mkono mkuu wa Israel katika vita dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa makadirio rasmi yaliyochapishwa, Marekani imetoa zaidi ya dola bilioni 22 za misaada ya kijeshi na silaha kwa utawala wa Kizayuni katika kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita. Katika muktadha huu, Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani lilikiri katika ripoti yake ambapo sambamba na kuashiria msaada mkubwa wa dola za Kimarekani bilioni 300 kwa Tel Aviv katika kipindi chote cha uhai wa utawala huo ghasibu lilitangaza kuwa, kama fedha hizo zingegawanywa kati ya watu milioni 30 wanaoishi chini ya mstari wa umaskini nchini Marekani, basi kila mtu angepata kiasi cha dola za Kimarekani 10,000.

Kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Hazina ya Marekani, nakisi ya bajeti ya nchi hiyo imefikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha uongozi wa Rais Joe Biden. Ofisi ya Bajeti ya Congress hivi karibuni iliandika katika ripoti yake:
Sababu kubwa katika ongezeko la ulimbikizaji wa deni ni sheria ambayo imepitishwa ambayo kimsingi imeongeza dola trilioni 1.6 katika nakisi iliyotabiriwa. Sheria hiyo inajumuisha matumizi ya dharura ya ziada yenye thamani ya dola bilioni 95 kusaidia Ukraine, Israel na nchi za eneo la Indo-Pacific.
Hali ngumu ya kiuchumi ya Marekani imemfanya Elon Musk, bilionea wa nchi hiyo na mmiliki wa Mtandao wa X, kuonya juu ya hali mbaya ya kiuchumi ya nchi hiyo. Musk alisema: Nchi yake inafilisika, na ikiwa mamlaka za Marekani hazitachukua hatua madhubuti, sarafu ya dola haitakuwa na thamani. Alisisitiza: Sauti za kengele ya hatari zinasikika kuhusu mustakabali wa kiuchumi wa Marekani.
Katika hali hii, Donald Trump Rais mteule wa Marekani, ameahidi kuboresha hali ya kiuchumi ya Marekani. Trump ambaye bado hajashika rasmi hatamu za uongozi wa nchi hiyo amezungumzia kuhusu vita vya ushuru wa forodha baina ya mataifa ya Ulaya na China, kufukuzwa wahamiaji haramu na kuendelea kuiunga mkono Israel, sera ambazo zinatathminiwa na weledi wa mambo kuwa, zinazoweza kuzorotesha zaidi hali ya kiuchumi ya Marekani.
Katika mazingira haya, wataalamu wa masuala ya kiuchumi wameonya kwamba, vita vya ushuru na mpango wa kufukuza mamilioni ya wahamiaji haramu utaongeza mfumuko wa bei nchini Marekani.