Muhammad; Jina pendwa na maarufu zaidi katika mji mkuu wa Ujerumani
Jina "Muhammad" limetangazwa kuwa ndilo jina pendwa na maarufu zaidi kwa watoto wa kiume katika miji ya Ujerumani ya Berlin na Brandenburg katika mwaka unaomalizika leo wa 2024.
Mtandao wa azon.global umeripoti kuwa, "Muhammad" linashika tena nafasi ya kwanza, kama jina pendwa na maarufu zaidi katika miji hiyo ya Ujerumani kama ilivyokuwa mwaka 2023, likifuatiwa na "Matteo" na "Elias."
Zaidi ya Waislamu milioni 5.5 wanaishi Ujerumani na wanaunda karibu asilimia 5 ya jamii ya watu wote nchini humo.
Azon Global pia imeripoti kuwa jina la Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, lilikuwa jina pendwa na maarufu zaidi nchini Uingereza na Wales mwaka wa 2023.

Mapema mwezi huu wa Disemba, Idara ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza ilitangaza kuwa jina "Muhammad" lingali ndilo jina linalopendwa kutumiwa zaidi nchini humo na wazazi kuwapa watoto wao wa kiume.
Kuanzia mwaka 2022, jina hilo la Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu lilipanda hadi nafasi ya pili katika orodha hiyo ya majina, lakini takwimu mpya zilizotolewa siku ya Alkhamisi na Idara ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza zimeonyesha kuwa jina "Muhammad" ndilo lililoshika nafasi ya kwanza mwaka 2023, likifuatiwa na jina la Nuh.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya kila wanaume 40 nchini Uingereza mmoja kati yao jina lake ni Muhammad.
Mapenzi ya kutumia jina la Mtume Muhammad (saw) kuwapa watoto wa kiume katika nchi za Ulaya yanazidi kuongezeka sambamba na kugonga mwamba sera za nchi za Magharibi zinazolenga kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kutoa taswira mbaya kuhusu Waislamu.