Shambulio la kisu Ujerumani, wawili wauawa
Watu wawili, yaani mtu mzima na mtoto mmoja, waliuawa katika shambulio la kudungwa kisu nchini Ujerumani jana Jumatano.
Maafisa katika eneo la tukio wameeleza kuwa, watu wawili wameuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa jana Jumatano baada ya kushambuliwa kwa kisu katika Bustani ya Aschaffenburg nchini Ujerumani.
Taarifa ya polisi ya Ujerumani imeeleza kuwa, wamefanikiwa kumtia mbaroni mshukiwa mmoja kufuatia hujuma hiyo ya kisu katika mji wa Aschaffenburg kusini mashariki mwa Bayern.
Katika upande mwingine, Idara ya Polisi katika eneo la Black Country huko Birmingham nchini Uingereza imetangaza kuwa imemtia nguvuni kijana mwenye umri wa miaka 14 kwa tuhuma za mauaji baada ya kufahamishwa kuhusu shambulio la kisu dhidi ya mvulana wa miaka 12.
Polisi imeeleza kuwa mtoto aliyeshambuliwa kwa kisu alianguka barabarani baada ya kujeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitalini, lakini jitihada za kuokoa maisha yake hazikufua dafu kutokana na majeraha aliyopata.
kKwa muda mrefu sasa wasiwasi umeongezeka kuhusu kupungua kwa umri wa wahalifu barani Ulaya hasa nchini Uingereza.
Ripoti zinaeleza kuwa katika kipindi cha karibu mwaka moja wa karibuni vijana 23 wameuawa katika jiji la London pekee na aghalabu ya mashabulio yalitekelezwa kwa visu na zana zingine kali.
Kituo cha Taifa cha Takwimu cha Uingereza hivi karibuni kilitangaza kuwa matukio ya uhalifu zaidi ya milioni 9 yameshuhudiwa nchini humo; kiwango ambacho ni cha juu zaidi katika historia ya nchi hiyo.