Karibu nusu ya Wadenmark wanaamini Marekani ni tishio kwa nchi yao
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya UGO ya nchini Uingereza yameonyesha kuwa asilimia 46 ya wananchi wa Denmark wanaamini kuwa Marekani ni tishio kuu kwa nchi yao.
Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yameonyesha kuwa asilimia 78 ya watu wa Denmark wanapinga kuuzwa eneo la Greenland kwa Marekani na asilimia 72 wanaamini kuwa eneo la Greenland lenyewe ndilo linalopasa kuchukua uamuzi kuhusu mustakbali wake na si serikali ya Denmark.
Uchunguzi huo wa maoni ulifanywa kati ya tarehe 15 hadi 22 mwezi Januari mwaka huu kwa kuwashirikia wananchi wa Denmark zaidi ya elfu moja.
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 7 mwezi Januari alitangaza kuwa Greenland ni lazima iwe sehemu ya Marekani ili kudhamimi usalama wa taifa wa nchi hiyo mbele ya vitisho vya China na Russia.
Mwaka 2019 pia akiwa katika muhula wake wa kwanza wa urais, Trump alipendekeza kununua kisiwa cha Greenland hata hivyo viongozi wa Denmark na Greenland walilitaja pendekezo hilo la Trump kuwa si la kimantiki.
Greenland ni eneo linalojitawala chini ya uongozi wa Denmark na tangu mwaka 1979 kisiwa hicho kina haki ya kuitisha kura ya maoni kuhusu mustakbali wa eneo hilo.