Ushuru wa Trump: Canada na Mexico zajibu mapigo, China yaonya
Canada, Mexico na China zimeapa kujibu mapigo ya uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani, wa kutoza ushuru wa juu kwa mataifa hayo matatu, na kuisukuma Washington katika vita vya kibiashara na nchi mbili jirani, na China yenye nguvu kubwa.
Siku ya Jumamosi, Trump alitangaza ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Canada, China, na Mexico, washirika watatu wakubwa wa kibiashara wa Marekani. Mexico na Canada zimeapa kulipiza kisasi kwa hatua hiyo ya Trump, wakati China ikisema itapinga hatua hiyo katika Shirika la Biashara Duniani na kuchukua "hatua zingine" za kujibu mapigo.
Saa chache baada ya hatua hiyo ya Trump, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ametangaza ushuru wa 25% kwa bidhaa za Marekani ambazo "zitajumuisha bidhaa za kila siku, kulipiza kisasi." Trudeau amesema, "Hatua ya Trump haitawadhuru Wacanada pekee, bali itakuwa na "matokeo halisi" kwa wananchi wa Marekani."
Kadhalika Rais Claudia Sheinbaum pia alitangaza jana Jumamosi kuwa, Mexico italipiza kisasi dhidi ya ushuru mpya uliowekwa na Trump kwa ushuru zaidi kwa bidhaa za Marekani, na hatua zingine zitakazoamuliwa baadaye.
Wakati huo huo, Beijing imetangaza leo Jumapili kuwa "inapinga vikali" ushuru uliowekwa na US dhidi ya Beijing, na kusisitiza kuwa itachukua "hatua zinazolingana ili kulinda kwa uthabiti haki na masilahi ya China."
Hivi karibuni pia, Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva alisema kuwa, "Iwapo Donald Trump atatoza ushuru kwa bidhaa za Brazil, tutachukua hatua sawa za kulipizia kisasi."