Ujerumani yakosoa vikali hatua ya Trump ya kuiwekea vikwazo ICC
(last modified Sat, 08 Feb 2025 11:48:22 GMT )
Feb 08, 2025 11:48 UTC
  • Ujerumani yakosoa vikali hatua ya Trump ya kuiwekea vikwazo ICC

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani amekosoa vikali hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Annalena Baerbock amesema katika taarifa yake kwamba "Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya sheria ya kimataifa ya uhalifu na inaungwa mkono na zaidi ya nchi 120."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani ameongeza kuwa, mahakama hii iliundwa misingi ya kanuni na kwamba inadhamini utekelezaji wa sheria za kimataifa za uhalifu na uhuru wa mahakama za kimataifa. Hii ndiyo sababu tunaunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na hii ndiyo sababu mahakama hii inahitaji msaada wetu.

Novemba mwaka jana (2024), ICC ilitoa waranti wa kukamatwa Netanyahu na waziri wake wa zamani wa masuala ya vita, Yoav Gallant kutokana na kutenda jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

 

Rais Donald Trump wa Marekani Alhamisi iliyopita alisaini agizo jipya la kuiwekea vikwazo mahakama ya ICC.  Trump alidai kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeingilia shughuli zilizo kinyume cha sheria na zisizo na msingi ambazo zimeilenga Marekani na mshirika wake wa karibu, utawala wa Kizayuni.

Nchi 79 duniani zimelaani vikwazo vya serikali ya Marekani dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya mjini The Hague, Uholanzi.

Novemba mwaka jana, ICC ilitoa waranti wa kukamatwa Netanyahu na waziri wake wa zamani wa masuala ya vita, Yoav Gallant. Hati hizo ni za "uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa kuanzia angalau Oktoba 8, 2023 hadi angalau Mei 20, 2024."