Trump: Canada 'haifai' kama nchi bila misaada ya Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani ameendelea kutoa kauli za dharau na kejeli dhidi ya nchi mbali mbali duniani, mara hii akiishambulia tena moja ya waitifaki wake, akisema Canada "haifai" kama nchi bila msaada wa kiuchumi na ulinzi wa kijeshi wa Marekani.
Kadhalika Trump amekariri pendekezo lake la kutaka Canada kujiunga na Marekani kama jimbo la 51, wazo ambalo serikali ya Ottawa inalipinga vikali. Kwa mujibu wa Trump, kuafiki kuwa jimbo la 51 la Marekani litakuwa "jambo kubwa zaidi ambalo [Canada] linaweza kufanya."
Rais huyo wa Marekani amedai kuwa, "Canada hailigharamii sana jeshi lake, na hii inatokana na wao kudhani kwamba tutawalinda ... hawalipi sehemu yao ya jeshi kwa NATO."
Trump ameendelea kubwabwaja kwa kusema: Jambo jingine ni kwamba, tunawapa ruzuku ya kiasi cha dola bilioni 200 kwa mwaka. Ikiwa tutaacha kufanya hivyo, na ikiwa hatutawaruhusu kutengeneza magari kupitia ushuru na vitu vingine - magari, lori, n.k., (Canada) haifai kabisa kama nchi."
Tangu aingie madarakani rasmi Januari 20, Trump amekuwa akiyatishia mataifa ya dunia kwa vikwazo, kukata misaada, na ushuru wa juu, zikiwemo hata nchi waitifaki wa Marekani.
Baada ya Trump kuiambia Canada kuwa atatoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za nchi hiyo zinazoingia Marekani, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau alijibu kivitendo hatua hiyo na kutangaza kuwa bidhaa za Marekani zinazoingia nchini humo nazo zitatozwa ushuru wa asilimia 25.