Mtaalamu wa Zambia: Ushuru wa Trump utawadhuru zaidi Wamarekani
Mtaalamu mmoja wa masuala ya biashara, ujasiriamali na uwezekaji wa Zambia amesema uamuzi wa serikali ya Marekani wa kutoza ushuru wa juu kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Canada, Mexico, na China utawadhuru zaidi Wamarekani.
Katika mahojiano na shirika la habari la Xinhua, Yusuf Dodia, msomi wa biashara na Mwenyekiti wa shirika la PSDA ameeleza bayana kuwa, "Hatua ya serikali ya Marekani ya kuongeza ushuru kwa bidhaa zinazotoka Canada, Mexico, na China hatimaye itawadhuru wanunuaji na watumiaji wa bidhaa hizo wa Marekani, kutoka na kuongezeka bei za bidhaa hizo katika nchi hiyo."
Ameongeza kuwa, uchumu wa Marekani unakabiliwa na mtikisiko mkubwa kutokana na vita hivyo vya kibiashara alivyoanzisha Trump, mara baada ya kushika usukani kuhudumu muhula wa pili. Dodia amesema akthari ya bidhaa zinazotoka Canada, Mexico na China hazitengenezwi nchini Marekani, na iwapo zinaundwa, hazikidhi mahitaji ya soko.
Tayari serikali za Canada, China na Mexico zimechukua hatua za kujibu mapigo kwa hatua hiyo ya Trump ya kuziongezea nchi hizo ushuru wa asilimia 25 kwa biadhaa zinazoingia Marekani kutoka nchi hizo tatu.

Mbali na Canada, China na Mexico, Trump ametishia kuiwekea Ulaya ushuru zaidi. Kufuatia vitisho hivyo vya Trump, viongozi wa EU karibuni walifanya mkutano mjini Brussels, na kujadiili tishio la ushuru la Marekani.
Kamisheni ya Ulaya imemuonya Trump kwamba "EU itatoa jibu kali kwa mshirika yeyote wa kibiashara ambaye anaweka ushuru usio wa haki au wa kiholela kwa bidhaa za jumuiya hiyo."