UN yalaani mashambulizi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi
(last modified Sun, 16 Feb 2025 07:52:03 GMT )
Feb 16, 2025 07:52 UTC
  • UN yalaani mashambulizi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imelaani mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi na kuutaka utawala huo kusitisha mara moja "wimbi la tahadhari ya machafuko na ukimbizi wa umati'' kwa raia wa Palestina.

Ofisi hiyo ya Haki za Binadamu ya UN imeashiria kuanza tena kuuawa kinyume cha sheria raia wa Palestina tangu Januari 21 mwaka huu na kutangaza kuwa askari usalama wa Israel kuanzia siku hiyo hadi sasa wamewaua raia wa Kipalestina 44; ambapo aghalabu yao hawakuwa na silaha wala kusababisha tishio lolote la haraka kwa utawala huo. 

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa: Mwamanke mjamzito ni kati ya raia waliouawa na Israel. Mwanamke huyo alikuwa akitafuta hifadhi baada ya mumewe kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama vya Israel pamoja na mtoto mmoja wa kiume wa miaka 10 ambaye alipigwa risasi  kifuani na askari wa Israel katika mji wa Tul Karam. 

Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN imeongeza kuwa imerekodi kuenea kwa matukio ya utumiaji nguvu kinyume cha sheria katika Ukingo wa Magharibi ambapo "hakuna mzozo unaoendelea," na utumiaji mabavu unaotajwa unaonyesha kuongezeka pakubwa mchakato wa raia wanaolazimika kuhama makazi yao kufutia mashambulizi ya utawala wa Kizyauni. 

Taarifa ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa ni marufuku kuwahamisha au kuwafukuza kwa nguvu wananchi wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kitendo hicho ni uhalifu kwa mujibu wa sheria za kimataifa; na Wapalestina waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na vita wanapaswa kuruhusiwa kurejea nyumbani.