Nusra Trump na Zelensky waparurane katika Ikulu ya White House!
Rais wa Marekani, Donald Trump na Makamu wake, JD Vance walitupiana vijembe na kushambuliana kwa maneno makali na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House jana Ijumaa.
Mkutano wa Ofisi ya Oval, ambao hapo awali ulipangwa kukamilisha makubaliano ya kuipatia Marekani haki ya madini adimu ya Ukraine, uligeuka na kuwa piga nikupige ya maneno baina ya viongozi hao wa Marekani na Ukraine.
Mvutano uliongezeka wakati Vance alipohimiza "diplomasia" kumaliza vita. Zelensky alipinga maoni hayo, akiuliza, "Ni aina gani ya diplomasia?" Swali hilo lilimfanya Vance kumshutumu Zelensy kwa "kutokuwa na heshima" katika Ikulu ya White House.
Wakimtuhumu Zelensky kwa kutoonyesha shukrani za kutosha kwa msaada wa Marekani kwa Kiev, Trump na Makamu wake JD Vance walipaza sauti zao, wakimshutumu Zelensky kuwa kizingiti katika njia ya makubaliano ya amani. "Kwa kweli hauko katika nafasi nzuri kwa sasa." Trump alisema na kuongeza, "Unacheza kamari na Vita vya Tatu vya Dunia."
Wakati mmoja kwenye vuta nikuvute hiyo, Vance alimshutumu Zelensky kwa "kutoheshimu" wenyeji wake wa Marekani. "Haufanyi hivyo kwa shukrani," Trump aliongeza. "Je, umewahi kusema 'asante' hata mara moja?" Vance alimuuliza Zelensky.
Fukuto lilipozidi katika Ikulu ya White House, Zelensky alitoka kwa hasira bila kujibu maswali ya waandishi wa habari. Mkutano huo uliisha ghafla, huku Trump akifuta pia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari uliokuwa umepangwa.
Zelensky aliondoka na msafara wake, na kuacha mpango wa madini bila kutatuliwa. Afisa wa Ikulu ya White House alithibitisha baadaye kuwa, hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa baina ya pande mbili hizo.