Zelenskyy akataa kuomba msamaha kwa Trump; Asema: "sikufanya lolote baya"
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123360-zelenskyy_akataa_kuomba_msamaha_kwa_trump_asema_sikufanya_lolote_baya
Rais wa Ukraine amekataa kuomba msamaha baada ya mabishano makali na majibizano ya maneno na mwenzake wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House.
(last modified 2025-03-01T10:07:59+00:00 )
Mar 01, 2025 10:07 UTC
  • Vuta nikuvute ya Trump na Zelenskyy
    Vuta nikuvute ya Trump na Zelenskyy

Rais wa Ukraine amekataa kuomba msamaha baada ya mabishano makali na majibizano ya maneno na mwenzake wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House.

Mkutano wa viongozi hao wawili katika Ofisi ya Oval, ambao hapo awali ulipangwa kukamilisha makubaliano ya kuipatia Marekani haki ya madini adimu ya Ukraine, uligeuka na kuwa piga nikupige ya maneno baina ya marais wa Marekani na Ukraine.

Fukuto lilipozidi katika Ikulu ya White House, Volodymyr Zelenskyy alitoka kwa hasira bila kujibu maswali ya waandishi wa habari. Mkutano huo uliisha ghafla, huku Trump akifuta pia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari uliokuwa umepangwa.

Akijibu swali la mtangazaji wa Fox News kuhusu iwapo anadhani kuwa ana deni la kuomba msamaha kwa Trump, Zelenskyy amesema: "Ninamheshimu Rais na watu wa Marekani. Nadhani tunahitaji kuwa wawazi na wakweli. Pamoja na hayo sina uhakika kwamba nimefanya jambo lolote baya."

Katika mkutano wa jana ndani ya White house, Rais Donald Trump na makamu wake, JD Vance, walimtuhumu Zelenskyy kuwa hakutoa shukrani za kutosha kwa msaada wa Marekani kwa Kiev. "Kwa kweli hauko katika nafasi nzuri kwa sasa." Trump alisema na kuongeza, "Unacheza kamari na Vita vya Tatu vya Dunia."

Zelensky aliondoka White House na msafara wake, na kuacha mpango wa madini bila kutatuliwa. Afisa wa Ikulu ya White House alithibitisha baadaye kuwa, hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa baina ya pande mbili hizo.