Manila yamkabidhi Rais wa zamani wa Ufilipino kwa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123804-manila_yamkabidhi_rais_wa_zamani_wa_ufilipino_kwa_icc
Takriban miaka mitatu baada ya kuachia ngazi, Rais wa zamani wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amekamatwa na mamlaka za nchi hiyo mjini Manila, kwa ombi la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ambayo inachunguza madai ya "uhalifu dhidi ya binadamu" unaodaiwa kufanywa na kiongozi huyo katika kipindi cha miaka sita alipokuwa madarakani.
(last modified 2025-03-12T07:05:58+00:00 )
Mar 12, 2025 07:05 UTC
  • Manila yamkabidhi Rais wa zamani wa Ufilipino kwa ICC

Takriban miaka mitatu baada ya kuachia ngazi, Rais wa zamani wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amekamatwa na mamlaka za nchi hiyo mjini Manila, kwa ombi la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ambayo inachunguza madai ya "uhalifu dhidi ya binadamu" unaodaiwa kufanywa na kiongozi huyo katika kipindi cha miaka sita alipokuwa madarakani.

Ndege iliyombeba Duterte, iliondoka Manila jana, saa chache baada ya ICC kutoa waranti unaomtuhumu kwa uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na "vita vyake dhidi ya dawa za kulevya."

Duterte, 79, aliwekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ninoy Aquino mjini Manila akitokea Hong Kong jana Jumanne.

Rais wa sasa wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr. amethibitisha kwamba Duterte ameondoka kwenye anga ya Ufilipino na anaelekea mjini The Hague nchini Uholanzi, ambako ICC ina makao yake.

Mahakama hiyo ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa inataka kumwajibisha Duterte kwa maelfu ya vifo vilivyotokea wakati wa kampeni yake ya kupambana na mihadarati, ambayo ilianza muda mfupi baada ya kuchukua madaraka mwaka wa 2016.

Kipindi cha Corona, Duterte alitoa amri ya kupigwa risasi wasiovaa barako

Licha ya maonyo aliyopewa kwamba atakuja kushtakiwa kwa kauli anazotoa hadharani kuhusu kuuliwa watuhumiwa wa mihadarati na kuhusu vita dhidi ya dawa hizo za kulevya, Rais huyo wa zamani wa Ufilipino alikuwa akizibeza indhari hizo za jamii ya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Duterte aidha ameshawahi kutangaza kwamba hajali chochote kuhusu haki za binadamu na akatoa amri ya kuwaua kwa kuwafyatulia risasi washukiwa wa mihadarati wanapokaidi kukamatwa.