Iran yamkosoa Mahmoud Abbas kwa kufanya kikao na MKO
(last modified Tue, 02 Aug 2016 07:27:02 GMT )
Aug 02, 2016 07:27 UTC
  • Iran yamkosoa Mahmoud Abbas kwa kufanya kikao na MKO

Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemkosoa vikali Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kufanya mazungumzo na mkuu wa kundi la kigaidi la Munafikina (MKO).

Muhsin Rezaei, Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema licha ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kufeli katika jukumu muhimu la kupiga hatua za maana kwa maslahi ya Wapalestina, lakini sasa ameamua kuunga mkono wazi wazi harakati za magaidi wa kundi la MKO lenye historia ya kufanya jinai nyingi na mauaji ya raia wasio na hatia ndani na nje ya Iran.

Muhsin Rezaei, Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Rezaei hata hivyo amesisitiza kuwa, njama na hatua yoyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasambaratishwa.

Jumamosi iliyopita, Mahmoud Abbas alikutana na kufanya mazungumzo na mkuu wa MKO Maryam Rajavi mjini Paris nchini Ufaransa, ambapo wawili hao walizungumzia matukio ya hivi sasa ya kieneo. 

Uhusiano wa karibu Munafikina na Marekani

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, mwezi uliopita wa Julai, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ilimuita Balozi wa Misri mjini Tehran kulalamikia hatua ya wabunge wa nchi hiyo ya kushiriki katika mkutano wa kundi la kigaidi la Munafikina (MKO) uliofanyika Paris mji mkuu wa Ufaransa, hivi karibuni.

Hamid Reza Dehqani, ofisa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema, Jamhuri ya Kiislamu inakosoa vikali hatua hiyo ya baadhi ya wabunge wa Misri kushiriki mkutano huo na kwamba kitendo hicho kinadhihirisha kuwa serikali ya Cairo inaunga mkono kundi hilo la kigaidi.