Wacanada waanza "kumtia adabu" Trump, bidhaa za Marekani zasusiwa Canada
Kuongezeka himaya na uungaji mkono wa Wacanada kwa bidhaa za nyumbani kumeibua wasiwasi kwa makampuni ya bidhaa mbalimbali ya Marekani.
Baadhi ya wauza rejareja wa Canada wameacha kuuza bidhaa za Marekani, hali ambayo imekuwa na athari za moja kwa moja kwa makampuni ya kigeni yanayouza bidhaa nchini humo.
Kuanzishwa vuguvugu la "Nunua Canada" (Buy Canada) kumezua wasiwasi miongoni mwa makampuni ya Marekani ambayo yanategemea kuuza bidhaa zao katika soko la rejareja la Canada.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa ununuzi wa bidhaa za ndani na kususiwa bidhaa za Marekani nchini Canada kumeongezeka kufuatia hatua za hivi majuzi za vita vya kibiashara za Rais wa Marekani, Donald Trump.
Sera za Trump, ikiwa ni pamoja na kutishia kuiunganisha Canada na kuifanya jimbo la 51 la Marekani, kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa chuma na alumini ya Canada na kutishia kuzidisha ushuru kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nchini humo, zimekabiliwa na mapigo makali kutoka kwa watumiaji wa Canada. Hali hii imepelekea kuongezeka hamu ya Wacanada ya kununua bidhaa za ndani ya nchi na kususia bidha kutoka Marekani.
Sasa makampuni ya Marekani yameanza kuhisi 'joto la jiwe' kutokana na kupungua mauzo yao nchini Canada.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu mpya wa Canada, Mark Carney ameamuru kupitiwa upya mkataba wa nchi hiyo na kampuni ya masuala ya ulinzi ya Marekani, Lockheed Martin, wa kununua ndege za kivita za F-35.