Polisi ya Uholanzi yakandamiza maandamano ya kuitetea Palestina
Makabiliano yaliripuka mjini Amsterdam kati ya polisi ya Uholanzi na waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina, wakati waandamanaji hao wakipita katika kitovu cha fedha cha mji huo, wakizituhumu kampuni kubwa kwa kujinufaisha kutokana na uhusiano wao na Israel wakati huu wa vita vinavyoendelea Gaza.
Press TV imeropoti habari hiyo leo na kueleza kuwa, waandamanaji hao wamesema kampuni kubwa za kimataifa zinatanguliza mbele faida na maslahi binafsi, huku Wapalestina wakikabiliwa na athari mbaya za vita hivyo katika Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji waliangazia kampuni katika sekta kama vile benki, utengenezaji wa silaha na tasnia zingine zinazodaiwa kushiriki katika kuwezesha au kufaidika moja kwa moja kutokana na mgogoro wa Gaza na ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina.
Kanda ya video iliyosambaa mitandaoni inaonyesha waandamanaji wakiwa wameshikilia mabango yenye ujumbe kama vile 'Hakuna Vyuo Vikuu vilivyosalia Gaza,' na 'Inatosha'.
Katika upande mwingine, makundi mbalimbali ya wananchi wa Uingereza yamefanya maandamano makubwa katika barabara za London, mji mkuu na miji mingine ya nchi hiyo kulaani mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.

Makundi tofauti ya wananchi wa Uingereza kwa mara nyingine tena yamefanya maandamano makubwa mno huko London na katika miji mingine ya nchi hiyo ili kulaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina hasa wa Gaza. Waandamanaji wameweka mashinikizo makubwa kwa serikali na wawakilishi wa majimbo ya Uingereza kuyataka yaache kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni.
Wananchi wa Uingereza wamesema: "Serikali yetu inaendelea kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na kuupa silaha; uungaji mkono huu lazima ukome."