Wizi wa kipochi cha Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani wazua kizaazaa
Ahadi za Donald Trump za kupunguza wizi na uhalifu nchini Marekani si tu ni ahadi chapwa, lakini pia watu wake muhimu ndani ya baraza la mawaziri nao hawajasalimika na wizi na uhalifu.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Christie Noemi ameibiwa kipochi chake wakati alipokuwa kwenye chakula cha jioni katika mkahawa mmoja mjini Washington.
Vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo tovuti ya habari ya televisheni ya CNN vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ndani ya kipochi hicho mlikuwa na pasipoti yake, beji ya usalama ya idara yake na pesa taslimu dola 3,000 za Kimarekani.
Kupanda gharama za maisha na kupungua uwezo wa manunuzi ya bidhaa kwa wananchi wa Marekani kumeongeza vibaka na kupandisha juu kasi ya wizi na vitendo vya uporaji nchini Marekani kwa asilimia 24. Maduka mengi sasa yameamua kuweka bidhaa zao kwenye vifurushi vilivyofungwa ili kukwepa wizi na uporaji na kukabiliana na vibaka.
Vita vya ushuru vilivyoanzishwa na Trump kote duniani katika wiki za hivi karibuni vimeongeza wasi wasi kuhusu hali mbaya ya uchumi nchini Marekani, na baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa kutokana na kupanda mfumuko wa bei, viwango vya wizi na uhalifu nchini Marekani vitaongezeka sana.