Polisi wa US wavamia nyumba za wanaounga mkono Palestina huko Michigan
(last modified Thu, 24 Apr 2025 10:38:02 GMT )
Apr 24, 2025 10:38 UTC
  • Polisi wa US wavamia nyumba za wanaounga mkono Palestina huko Michigan

Maafisa usalama wa serikali ya shirikisho ya Merekani wamefanya uvamizi ulioratibiwa kwenye makazi ya wanaharakati wanaounga mkono Palestina wanaohusishwa na Chuo Kikuu cha Michigan.

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, maafisa hao wamewazuilia na kuwahoji wanaharakati wengi watetezi wa Palestina katika uvamizi huo, mbali na kukamata vifaa vyao vya kielektroniki na mali zao za kibinafsi.

Shirika la Wafanyikazi Waliohitimu (GEO) limesema operesheni hiyo, iliyofanywa na Polisi ya Upelelezi (FBI), Polisi wa Jimbo la Michigan, na askari wa idara za mitaa, ililenga nyumba za wanaharakati hao katika maeneo ya Ann Arbor, Ypsilanti, na Canton. Vyanzo vya habari vimesema kuwa, uvamizi huo ulitekelezwa kutokana na agizo la Mwanasheria Mkuu wa Michigan, Dana Nessel.

Muungano wa GEO umeshutumu vikali uvamizi na ukandamizaji huo. "Tunalaani vikali hatua zilizochukuliwa za ukandamizaji hii leo na huko nyuma, dhidi ya harakati za kisiasa."

Muungano huo umetoa wito wa kuwajibishwa na kubebeshwa dhhima maafisa wa Chuo Kikuu cha Michigan na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa jimbo hilo kwa kutoa amri ya kutekelezwa ukandamizaji huo.

Uvamizi huo ni sehemu ya kampeni pana ya nchi nzima ya kukandamiza wanaharakati wanaoitetea Palestina, haswa kwenye Vyuo Vikuu.

Katika miezi ya hivi karibuni, maandamano ya wanafunzi, na mikusanyiko ya kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na kujitenga kutoka kwa Israel kumekabiliwa na uchunguzi unaoongezeka, na vyuo vikuu vingine vikisimamisha wanafunzi na kughairi hafla.

Utawala wa Donald Trump pia umezidisha uchunguzi, mbinyo na ukandamizaji dhidi ya makundi yanayounga mkono Palestina. Wakosoaji wanasema hatua hizi zinakiuka uhuru wa kujieleza na kulenga upinzani dhidi ya sera ya kigeni ya Marekani. 

Zaidi ya marais 100 wa Vyuo Vikuu na taasisi za elimu karibuni walitoa taarifa ya pamoja wakipinga sera za utawala wa Trump kwa taasisi za elimu ya juu, baada ya Chuo Kikuu cha Harvard kusema utawala huo unatishia uhuru wake.