Kulaani nchi za Ulaya hatua ya Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu Gaza
(last modified Sat, 03 May 2025 02:16:05 GMT )
May 03, 2025 02:16 UTC
  • Kulaani nchi za Ulaya hatua ya Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu Gaza

Huku mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yakiendelea na hali ya mambo katika eneo hilo kuwa mbaya zaidi, Uhispania, Ubelgiji na Ireland, nchi tatu wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekosoa vikali kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kukiuka usitishaji vita na kuanzisha tena mashambulizi katika Ukanda wa Gaza.

Mataifa hayo yamelaani hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kutumia misaada ya kibinadamu kama silaha dhidi ya Gaza.

Mwakilishi wa Kudumu wa Uhispania katika Umoja wa Mataifa, Hector Gomez Hernandez, alisema Jumatano, Aprili 30, katika mjadala wa wazi kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Palestina, kwenye Baraza la Usalama: "Kurejeshwa mashambulizi huko Gaza na kushadiidi operesheni za kijeshi katika Ukingo wa Magharibi kunazidisha hali mbaya ya hali ya kijeshi ambayo pia inalenga wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu."

Ameyataja mashambulizi hayo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kulaani ukiukaji wa usitishaji vita kati ya Israel na Hamas.

Sophie De Smedt, mwakilishi wa kudumu wa Ubelgiji katika Umoja wa Mataifa, pia alisema katika taarifa yake: "Tunataka kukomeshwa ukiukaji wa sheria za kimataifa." Misaada isigeuzwe kuwa silaha katika mzozo huu. Akisisitiza kuwa msaada wa kibinadamu hauwezi kujadiliwa, alitoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa vikwazo vya misaada, kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kulazimishwa kumaliza shughuli zao huko Gaza, na mashambulizi dhidi ya shughuli za kibinadamu.

Zaidi ya Wapalestina 60,000 wameuawa shahidi tangu Isael iliipoanzisha hujuma yan kinyama dhidi ya Gaza 2023

 

Afisa huyo wa Ubelgiji sanjari na kuutaka utawala wa Israel ukubali kuingizwa misaada ya kibinadamu huko Gaza alisema: "Sheria za kimataifa za haki za binadamu lazima ziheshimiwe na pande zote kwa hali yoyote." Ndivyo ilivyo kuhusu kanuni za msingi za kibinadamu za kutopendelea, uhuru, na ubinadamu.

Fergal Mythen mwakilishi wa kudumu wa Ireland katika Umoja wa Mataifa, pia alisema: "Tunachoshuhudia huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kinaonyesha kutoheshimiwa kabisa sheria za kimataifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na uadilifu wa Umoja wa Mataifa kama taasisi." Amebainisha kuwa, kuendelea kupinga utawala wa Israel kupelekwa misaada ya kibinadamu na bidhaa za kibiashara huko Gaza kunazidisha kasi mgogoro wa njaa katika eneo hilo.

Mythen alisisitiza: Ireland inalaani kuanzishwa tena mashambulizi ya anga ya Israel na operesheni za ardhini huko Gaza, ambazo zimeleta mateso mapya kwa watu wa eneo hilo na kukiuka usitishaji mapigano.

Hali ya Gaza sasa imekuwa mbaya sana kiasi kwamba Umoja wa Mataifa umeonya waziwazi kuhusu hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliambia Baraza la Usalama: "Hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza imezidi kuwa mbaya zaidi na kupita ilivyodhaniwa." Kwa takriban miezi miwili kamili, Israel imezuia chakula, mafuta, dawa na vifaa vya kibiashara, na kuwanyima zaidi ya watu milioni mbili misaada muhimu.

Tuukitupia jicho misimamo ya nchi za Ulaya kuhusiana na vita vya Gaza na kuendelea mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya watu wa Gaza tunashuhudia  mgawanyiko wa wazi uliopo baina ya nchi hizo katika suala hili, ambalo bila shaka chimbuko lake ni mitazamo na utendaji tofauti wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu kadhia ya Palestina.

Baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Uhispania, Ireland na Ubelgiji zimetoa wito kwa uwazi juu ya kutambuliwa taifa la Palestina na zimechukua msimamo wa kulaani vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza. Wakati washirika wa karibu wa Marekani barani Ulaya, kama vile Ujerumani na Austria, na nchi za Ulaya Mashariki, kama vile Jamhuri ya Czech na Hungary, zimechukua msimamo wa kuunga mkono Israel, na zinaunga mkono kuendelea operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya Wapalestina kwa kisingizio cha kujilinda, na hata Ujerumani inaendelea kutuma silaha kwa utawala huo wa Kizayuni.

 

Kutokana na misimamo ya karibu na kuwa pamoja baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani kwa upande mmoja, na kuwepo lobi za Wazayuni katika nchi hizo, kimsingi ni jambo lisilowezekana kwao ni kubadili misimamo yao na kushika nafasi ya kati na kati, mbali na misimamo ya undumakuwili kuhusiana na utawala wa Kizayuni na Wapalestina.

Pamoja na hayo misimamo iliyochukuliwa na baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Israel ya kulaani mauaji ya halaiki na utumiaji njaa kama silaha na kuzuia kutumwa misaada ya kibinadamu na utawala wa Kizayuni wenye lengo la kuwaangamiza watu wa Gaza na kuwalazimisha kuondoka Gaza, ni mambo yanayobashiri kwamba, muda wa uungaji mkono wa pande zote kwa Israel umefikia tamati, hata miongoni mwa nchi za Ulaya, na Tel Aviv inazidi kupoteza nguvu zake laini na uwezo wa kushawishi maoni ya umma katika nchi za Magharibi, hasa za Ulaya na Marekani, ili kuhalalisha vitendo vyake vya jinai dhidi ya watu wanaokandamizwa wa Gaza.