Zakharova: Ukraine haitakuwa salama kutokana na mauaji ya waandishi habari wa Russia
-
Maria Zakharova
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa Kiev inatumia mbinu na vitendo vya kigaidi kuwaua waandishi wa habari wa Russia na haitasalimika katika suala hili.
Akieleza kwamba nchi za Magharibi zimenyamaza kimya kuhusiana na mauaji ya wafanyakazi wa vyombo vya habari vya Russia, Maria Zakharova amesema kuwa Kiev inavilenga vyombo vya habari na waandishi wa habari wa Russia kwa kila aina ya ukandamizaji na mashambulizi kwa kisingizio cha kupambana na usambazaji wa habari feki.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia amesema kuwa tangu Februari 2022, makumi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari wameuawa au kujeruhiwa na askari wa Kiukreni.
Zakharova amesisitiza kuwa Kiev inatumia mbinu za kigaidi kutekeleza mipango hiyo ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari wa Russia.
Amesema kuwa wale waliohusika na mauaji ya waandishi wa habari wa Russia lazima wapate adhabu kali, na kwamba msaada wa nchi yoyote ya Magharibi hauwezi kuzuia adhabu hiyo kutekelezwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametoa wito kwa mashirika kama UNESCO, Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na mengine kulaani bila masharti uhalifu huo wa kinyama.