Wataalamu wa Vatican: Papa ajaye aliunganishe Kanisa kutokana na mpasuko mkubwa uliopo
(last modified Tue, 06 May 2025 06:15:07 GMT )
May 06, 2025 06:15 UTC
  • Wataalamu wa Vatican: Papa ajaye aliunganishe Kanisa kutokana na mpasuko mkubwa uliopo

Wakati Kanisa Katoliki linajiandaa kwa mkutano wa kumchagua Papa mpya utakaoanza kesho Jumatano, wachambuzi wa Vatican wanasema, makadinali wako chini ya mashinikizo ya kumchagua papa mwenye uwezo wa kuziba mgawanyiko unaoendelea kukua kati ya pande mbili kuu za wanamageuzi na wahafidhina ndani ya Kanisa hilo.

Kipindi cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francis aliyefariki tarehe 21 Aprili kilimalizika tarehe 4 Mei. Macho yote sasa yanaelekezwa kwa Chuo cha Makadinali kitakachokusanyika katika Kanisa la Sistine kesho Mei 7 kumchagua Papa ajaye.
 
Marco Politi, mwandishi wa habari wa Italia anasema, mkutano huo utakuwa wa aina yake kwa sababu katika kipindi cha miaka 50, Kanisa Katoliki halijawahi kugawanyika kama ilivyo sasa.
 
Kwa mujibu wa Politi upapa wa kimageuzi wa Papa Francis, uliothibiti kwa kuzifikia jamii zilizotengwa na kutoa msukumo juu ya masuala ya uwazi na uwajibikaji, ulikabiliwa na upinzani ambao ungali unaendelea kutoka kwa makundi ya kihafidhina.
Katika ujumbe wake wa mwisho wa hadhara kabla ya kifo chake, Francis alikiri kuwepo kwa mivutano hiyo na akahimiza juu ya umoja.
 
Majina yaliyotajwa katika duru za Vatican ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin, Patriaki Pierbattista Pizzaballa, na Kadinali Matteo Maria Zuppi, miongoni mwa wengine. Politi anabainisha kuwa kabla ya uamuzi wowote kufanywa, itapasa makadinali wakubaliane kwanza juu ya mada na vipaumbele ambavyo vitaainisha mwelekeo wa Kanisa.
 
Mwandishi mwingine wa habari wa Italia Giovanna Chirri, ambaye alitangaza habari ya kujiuzulu kwa Papa Benedict XVI mwaka 2013, yeye anasema mkutano huo wa kumchagua papa mpya utafanyika katika wakati muhimu sana.
 
Chirri anasisitiza kuwa, "Papa ajaye lazima aendeleze urithi wa Francis huku akiunganisha makundi mbalimbali".
 
Mwandishi huyo anaitakidi kuwa ikiwa katika makutaniko yao, makadinali wataweza kufikia makubaliano juu ya masuala ya kushughulikiwa, basi wanaweza kupata jina la papa mpya haraka ndani ya kipindi cha siku 3 hadi 4.../