Kanisa Katoliki lapata Papa mpya, ni Kadinali Robert Prevost atakayejulikana kama Leo XIV
(last modified Fri, 09 May 2025 03:04:10 GMT )
May 09, 2025 03:04 UTC
  • Kanisa Katoliki lapata Papa mpya, ni Kadinali Robert Prevost atakayejulikana kama Leo XIV

Kanisa Katoliki duniani hatimaye limepata kiongozi mpya ambaye ni Kadinali Robert Francis Prevost atakayejulikana kama Leo XIV.

Baada ya majadiliano yaliyochukua muda wa siku mbili, mkutano wa siri wa kumchagua Papa uliofanyika katika kanisa la Sistine mjini Vatican ukijumuisha makadinali 133 kutoka mataifa 70 duniani, Alkhamisi jioni ulimtangaza Kadinali Prevost, mwenye umri wa miaka 69 kuwa kiongozi mpya wa kanisa katoliki kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Papa Francis, aliyefariki Jumatatu ya Pasaka Aprili 21 akiwa na umri wa miaka 88.

Leo XIV, ambaye anakuwa Papa wa kwanza raia wa Marekani alizaliwa Chicago Septemba 14, 1955. Prevost alisoma katika Umoja wa Kitheolojia wa Kikatoliki wa Chicago, akitunukiwa diploma ya theolojia.

Akiwa na umri wa miaka 27, alikwenda Roma kusomea sheria za kanuni katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas. Mafunzo yake ya kidini yalimfikisha Peru kama mmishionari, na baadaye akafanikiwa kupata nyadhifa mbalimbali nchini Marekani na Peru akiwa na uraia wa nchi hiyo pia.

Alipotokeza hadharani kwa mara ya kwanza hapo jana na kuhutubia kwa Kiitaliano umati uliokuwa ukishangilia Papa Leo XIV alisema: "Amani iwe nanyi nyote".

Aidha, alitoa shukrani kwa mtangulizi wake, Papa Francis, huku akisema anataka kuwasilisha baraka zake kwa watu kama Papa Francis alivyofanya mara ya mwisho alipojitokeza katika uwanja wa St Peter's Square.

Kiongozi huyo mpya wa Kanisa Katoliki lenye wafuasi wapatao bilioni 1.4 duniani aliwashukuru pia makadinali waliomchagua wakati wa mkutano wa siku mbili.../