Makamu wa Rais wa Marekani: Vita vya India na Pakistan 'havituhusu'
(last modified Fri, 09 May 2025 07:47:00 GMT )
May 09, 2025 07:47 UTC
  • Makamu wa Rais wa Marekani: Vita vya India na Pakistan 'havituhusu'

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema, nchi hiyo haitaingilia mzozo kati ya India na Pakistan.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Fox News, Vance amesema: "tunataka mvutano huu upungue haraka iwezekanavyo. Hata hivyo, hatuwezi kuzidhibiti nchi hizi".
 
Makamu huyo wa rais wa Marekani ameendelea kueleza: "tunachoweza kufanya ni kujaribu kuwahimiza watu hawa wapunguze mvutano, lakini hatutajihusisha na vita ambayo kimsingi havituhusu na haviendani kwa namna yoyote na uwezo wa Marekani wa kuvidhibiti".
 
Aidha, amesema Marekani haiwezi kuulazimisha upande wowote "kuweka silaha chini," na akongeza kuwa nchi hiyo "itaendelea kufuatilia suala hilo kupitia njia za kidiplomasia."
 
"Matumaini yetu na matarajio yetu ni kwamba hili haitaingia kwenye vita vya kikanda au, Mungu aepuishe mbali, mzozo wa nyuklia," amesema makamo wa rais wa Marekani.
 
Mzozo wa makabiliano ya kijeshi kati ya India na Pakistan umechochewa na shambulio la kigaidia la Aprili 22 katika eneo la Pahalgam, kwenye jimbo la Kashmir inayotawaliwa na India, ambapo watu 26 waliuawa.
 
India iliilaumu Pakistan kwa shambulio hilo, ikidai kuwa ilihusika nalo, tuhuma ambayo Pakistan imeikana na kutaka ufanyike uchunguzi huru kubaini chimbuko la shambulio hilo, takwa ambalo India imelikataa.../