Witkoff: Amani haiwezi kupatikana Ukraine bila ridhaa ya Putin
(last modified Wed, 14 May 2025 02:44:34 GMT )
May 14, 2025 02:44 UTC
  • Witkoff: Amani haiwezi kupatikana Ukraine bila ridhaa ya Putin

Steve Witkoff, Mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani, Donald Trump amesema utatuzi wa amani wa mzozo wa Ukraine hauwezekani bila idhini na ridhaa ya Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani, kuwepo mawasiliano na Shirikisho la Russia ni muhimu katika kutatua mzozo wa Ukraine.

Witkoff amebainisha kuwa, Trump anasisitiza juu ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Russia na kuipa Ukraine "muhula wa mwisho," vinginevyo Marekani itajiondoa katika mchakato wa kutafuta suluhu.

Mjumbe huyo maalumu wa Trump ametaja mada kuu za mazungumzo hayo kuwa ni Kyiv kusalimisha baadhi ya maeneo, matumizi ya Kiwanda cha Nyuklia cha Zaporizhzhia, na Ukraine kuruhusiwa kufikia Mto Dnipro na Bahari Nyeusi.

"Mengi tayari yamefanywa kupunguza msururu wa matatizo. Mazungumzo yasiyo rasmi yanafanywa na Moscow na Kyiv," Witkoff amesisitiza.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais wa Russia kutoa wito akitaka kuanza tena mazungumzo ya moja kwa moja bila masharti kati ya nchi yake na Ukraine mjini Istanbul, Mei 15, ili kufikia makubaliano ya amani ya kudumu.

Putin amesema kuwa uamuzi sasa upo upande wa mamlaka husika za Ukraine ambao inaonekana, wanaongozwa na matashi ya kibinafsi ya kisiasa, na sio maslahi ya watu wao.

Dmitry Peskov, Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) amesema kuwa 'hili ni pendekezo muhimu sana, ambalo linathibitisha nia ya kweli ya Moscow kupatikana suluhisho la amani.”